NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SERIKALI imesema haina dini,hivyo itaendelea kushirikiana na madhehebu yote ya dini na kuwahudumia wananchi kwa haki na kuwataka wazazi na walezi kusimamia malezi na elimu ya watoto wao wawe na maadili mema.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda,amesema leo wakati akizungumza katika Baraza la Eid El Fitr,lililofanyika katika Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania (BOT),Capripoint jijini humu.
Amesema serikali ingawa haina dini lakini itawahudumia kwa haki wananchi wa madhehebu yote na wasio na dini,katika kujenga maadili mema kwa vijana wazazi na walezi watimize haki na wajibu wao wa kusimamia malezi bora ya watoto kwani maadili huanzia nyumbani.
“Niwakumbushe wazazi na walezi,mmesahau kutimiza haki na wajibu wa malezi ya watoto.Jamii bora itajengwa na vijana bora, hawawezi kupatikana kama hawana malezi bora.Hivyo,wazazi na jamii mnawajibika kuwajenga vijana na kuwafanya wawe na adabu,”amesema Mtanda na kuongeza;
“Tusimamie elimu na maadili mema kwa vijana na watoto wetu.Mtu yeyote aliyekosa elimu na adabu ni yatima,tusiwafanye vijana yatima kwa kukosa elimu na adabu,tuwape elimu ambayo ni kichocheo cha maisha bora ya binadamu aliyeandaliwa vizuri.”
Mkuu huyo wa mkoa amesema vijana (Waraibu) wanaotumia dawa za kulevya wengi walikosa malezi ya wazazi wote wawili wakihangaika kutafuta kupata fedha nyingi na kusahahu waji wao pia,wasichana wa kiislamu wasijiingize na kuona fahamu kujiita single mother.
Kufunga Ramadhani
Amesema kufunga Ramadhani kuna faida kubwa, moja ni kumcha Mungu na nyingine za kidunia ikiwemo kutunza afya,kuimarisha upendo na uhusiano miongoni mwa waislamu,kuwafanya wakarimu hasa wasio waislamu na mikusanyiko hiyo imeleta neema kwa watu wengine.
“Tumepokea maelekezo ya Mufti kuwa tuliyofanya na tuliyojifunza ndani ya Ramadhani tuyaendeleze,yameleta mshikamano miongoni mwa waislamu na wasio,wenye mioyo ya chuki na roho mbaya wamekuwa na roho za ukarimu,wenye jazba watakuwa watu wema na wacha Mungu,”amesema Mtanda.
Ameipongeza BAKWATA Mwanza na waislamu,kujenga vituo vya afya akisema ndiyo sababu Rais Dk.Samia anajenga vituo vingi tutunze na tuimarishe afya zetu,hivyo atatoa ushirikiano hadi vikamilike.
“Muumini mwenye afya njema mbele ya Mungu ni bora kuliko mdhaifu.Sura al-Baqarah aya ya 10 inasema; kuna watu wana maradhi katika nafsi zao,wana macho lakini hawaoni,wana masikio hawasikii.Tuwe miongoni mwa watu wanaosikia yale yanayosemwa na viongozi wetu,tuyapokee na kuyazingatia,”amesema Mtanda.
Pia amewashukuru viongozi wa dini na waumini kumwombea Rais Dk.Samia huku akiwaasa kumtii Mungu na waliochaguliwa naye na mamlaka zilizopo kwani hakuna mamlaka haikuwekwa na Mungu,hata zisizo na uadilifu zimewekwa ili kuwapima .
“Neema ikizidi unaweza kukufuru.Wengine walidhani atashida kuongoza nchi na tunawajibu wa kumwombea,tunapomwombea Rais afya njema ikiyumba, nchi nayo inayumba na tunamwombea ametutendea wema wala hamfanyi makosa ni ni maelekezo ya vitabu vya dini,”amesema Mtanda.
Kulipa kodi
Amesema kulipa kodi ni wajibu na hata zamani ilikuwepo hivyo si suala la Rais Dk.Samia,na nchi isiyokusanya kodi kiuchumi italega lega kwa kuwa ni mtu wa maamuzi ya haki na si wa matumizi ya nguvu atasimamia hilo mkoani Mwanza.
“Katika utendaji wangu sina mpambe,mpambe ni utendaji wangu.Nitasimamia ukusanyaji wa kodi kwa haki,wakwepa kodi hao si rafiki zangu,lakini wanaodhulumiwa na kutaka kufunga biashara na wako tayari kulipa kodi,nitawaunga mkono,”amesema Mtanda.
Awali Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke,amesema BAKWATA ni daraja kati ya waislamu na serikali yao,hivyo siku ya Baraza la Eid ni siku ya serikali kuelekeza masuala mbalimbali yanayohusu wananchi.
“Mgeni rasmi ujumbe wa Mufti Abubakar Zuber Bin Ali Mbwana kupitia hadhira hii ni kuendeleza mazuri tuliyoyaishi ndani ya Ramadhani.Ewe Mtanzania endelea kulipa Kodi kwa Maendeleo ya Taifa ukiwa ni ujumbe wa Rais Dk.Samia na Shiriki Uchaguzi Mdogo wa Serikali za Mitaa 2024.Ujumbe huo kupitia hotuba za viongozi hao Waislamu wa Mwanza tumezipokea,”amesema Sheikh Kabeke.