RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Naibu Mifti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Mahmoud Mussa Wadi alipowasili katika viwanja vya Masjid Hidaya Kilimani Tazari Kidoti Mkoa wa Kaskazini Unguja, kuhudhuria Ibada ya Sala ya Ijumaa na Kisomo cha Hitma na Dua ya kumuiombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Pili Mstaafu Hayati Alhajj Ali Hassan Mwinyi, iliyofanyika leo 12-4-2024.(Picha na Ikulu)
……………………
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi ametoa shukrani zake za dhati kwa wananchi na viongozi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa kuendelea kumuombea du’a na khitma baba yake Mzazi Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi aliefariki hivi karibuni.
Al hajj Dk. Mwinyi, ametoa shukurani hizo mara baada ya ibada ya sala ya Ijumaa iliyofuatiwa na visomo mbalimbali, hitma na du’a kweye masjid Hidaya, Kilimani Tazari, Mkoani humo.
Akizungumza kwa niaba ya Familia yake, Al hajj Dk. Mwinyi amewashukuru wananchi hao kwa mapenzi yao kwa Mzee Mwinyi tangu walipomuuguza hadi alipokufa Februari 29 mwaka huu.
Naye, Mkuu wa Mkoa huo, Rashid Hadid Rashid alisema wanachi wa Kijiji cha Kilimani Tazari na vijiji jirani, kwa makusudi waliamua kukaa pamoja kumuombea du’a Marehemu Mzee Ali Hassan Mwinyi, viongozi waliopo hai na wazee wa vijiji hivyo waliofariki dunia.
Akizungumza kwenye ibada hiyo, Sheikh Khamis Abdul Hamid aliwahusia waumini wa kiislam kuendelea kufanya mema na kumcha Mwenyezi Mungu kwa haki ili roho zao zikawekwe mahala pema baada ya kufa.
Mapema akikhutubu kabla ya sala ya Ijumaa, Khatib Sheikh, Omar Abdi aliwasihi wananchi na waumini wa dini ya Kiislam kuendelea kujenga hofu kwa Mwenyezi Mungu kwa kukithirisha ibada hata baada ya kumalizika kwa Mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Aliusia kwamba Mwenyezi Mungu hayupo Mwezi wa Ramadhan pekee bali yupo siku zote, hivyo aliwanasihi waumini hao, kuendeleza ibada kwa siku za kawaida kama ilivyokuwa Ramadhan.
Ibada hizo za visomo na du’a na hitma pia waliombewa viongozi waliopo serikalini, wastaafu, masheikh na wazee walio hai na waliotangulia mbele ya haki ndani na nje ya Mkoa huo.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali akiwemo Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh, Saleh Omar Kaab, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Rashid Hadid na viongozi wengine.