NA VICTOR MASANGU,KIBAHA
BAADHI ya wanachama na viongozi wa chama cha mapinduzi na wananchi wa Kata ya Msangani wamempongeza kwa dhati Mwenyekiti wa CCM Kibaha mji Mwajuma Nyamka kwa upendo wake wa kuwakutanisha kwa pamoja katika kusherekea sikukuu ya Iddy mosi nyumbani kwake.
Baadhi ya viongozi hao akiwemo Diwani mteule wa kata ya Kata ya Msangani Gunze Yohana ambaye amechaguliwa hivi karibuni kwa kishindo cha asilimia 99.20.
Gunze aliongeza kuwa amefanya jambo la upendo la kuamua kuwakutanisha baadhi ya wanachama,viongozi na wananchi ili kuweza kujumuika katika chakula cha mchana katika kusherekea sikukuu ya Iddy mosi.
“Kiukweli Mwenyekiti wetu wa chama ameonyesha upendo maana kitendo tu cha kutukutanisha nyumbani kwake sisi kiukweli tumefarijika na Mungu ambariki kwa moyo wake wa kujitolea ,”alisema Gunze.
Naye balozi wa mtaa wa Kidenge Said Mbunju alisema kwamba Mwenyekiti Nyamka amekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na jamii na kwamba amefarijika sana kushiriki chakula cha mchana nyumbani kwa Mwenyekiti.
“Nafahamu leo hii ni sikukuu lakini sisi tumekuja kwa niaba ya wengine lakini nipende kuchukua fursa hii kumshukuru kwa moyo wangu wote maana tumeweza kukutana na kubadilishana mawazo mbali mbali “,alisema Said.
Mjumbe huyo alisema katika sikukuu watu wengi wamekuwa wakikutana na ndugu zao lakini kwa upendo wa Mwenyekiti akaona akutane na jamii ili kuweza kula chakula cha mchana sambamba na kubadilishana mawazo.
Kwa upande wake Mwenyekiti huyo wa CCM Kibaha mji aliwahimiza viongozi na wanachama wa ccm kuhakikisha wanakuwa na umoja na upendo kipindi chote.
Nyamka alisema kwamba anatambua kwamba katika siku za siku kuu kila mtu anakuwa na majukumu mengi lakini akaona awashirikishe baadhi ya watu ili aweze kujumuika nao katika chakula cha mchana.
“Mimi kiukweli nawashukuru wale wote ambao baadhi yao niliwaomba tujumuike kwa pamoja na wote mimi ninawapenda japo niliita baadhi tu kwa niaba ya wengine Mungu awabariki sana,”alisema Nyamka.
Kadhalika Nyamka pamoja na kuwapongeza aliwakumbusha viongozi na wana ccm kwa ujumla umuhimu wa kuhakikisha kwamba wanajipanga vizuri katika kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.
Mwenyekiti huyo wa CCM Kibaha mji ametumia sikukuu ya Iddy mosi kuwakaribisha baadhi ya viongozi wa ccm,wanachama na wananchi lengo ikiwa ni kula chakula cha mchana pamoja na kubadilishana mawazo.