Ashrack Miraji Same Kilimanjaro
Same.Waislamu nchini Tanzania wamehimizwa kusherekea sikukuu ya Eid El Fitri kwa kutenda matendo mema,wakitahadharishwa kutofanya zinaa,kunywa pombe na kukesha kwenye kumbi za starehe kwani kwa kufanya hivyo funga yao itahesabika kutokuwa na maana.
Nasaha hizo zimetolewa leo Aprili 10,2024 na Sheikh Abubakar Harid wakati akitoa hotuba ya swala ya Eid El Fitri iliyofanyika katika msikiti wa Masjid Nuru uliopo Wilaya ya Same Mkoani Kilimanjaro.
Amesema ni vyema waislamu wakaitumia sikukuu hii kwa kutenda mambo mema,pia kukumbushana kuwaombea dua ndugu walio tangulia mbele ya haki na kuachana na vitendo viovu vya kunywa pombe,uzinifu na kukesha kwenye kumbi za starehe.
Sheikh Harid amesema kwamba aina hiyo ya usheherekeaji wa sikukuu ya Eid El Fitri ambao haumpendezi Mungu na Mtume wake Mohammad S.A.W na kwamba,Uislamu ni dini inayowataka watu siku hii kutembelea Ndugu,marafiki,Kula na kunywa vyakula vya halali.
“Niwakumbushe waislamu wote kuwa sikukuu hii ya Eid El Fitri iwe sikukuu njema ya kutenda mambo mema na kuwaombea dua ndugu zetu waliotangulia mbele ya haki,pia tuachane kabisa na vtendo viovu vya kunywa pombe, uzinifu na kukesha kwenye kumbi na majumba ya starehe”
“Ni heri ukasheherekea sikukuu hii vizuri kama ulivyokuwa ukifanya kwenye kipindi Cha mfungo wa Ramadhani ambacho kilikuzuia wewe usifanye anasa na Mwenyezi Mungu ametuambia kwenye vitabu kwamba siku ya Eid iwe siku ya kutembelea ndugu, marafiki, kula na kunywa vyakula halali na kuacha kunywa na kula vyakula haramu”
Aidha Sheikh huyo ametumia fursa hiyo kuwasihi wananchi wa Kilimanjaro kuwaombea dua viongozi wote wa serikali hasa wa Kitaifa akiwemo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan na Mkuu wa Wilaya ya Same,Kasilda Mgeni,kwani viongozi hao wamekuwa chachu ya maendeleo wilayani hapo ambapo sasahivi Same ni moja ya Wilaya ambayo ni kitovu cha utalii nchini.
“Mkuu wa Wilaya ya Same Kaslida Mgeni anatupa sana ushirikiano mkubwa hasa Kwa taasisi za dini wilayani kwetu katuweka pamoja,tumejadili masuala mbalimbali ya kuliongoza Taifa letu,pia ametualika mara kadhaa kwenye lftar na kushirikisha taasisi zote za kidini”
“kipindi hicho chote tulikuwa kwenye mfungo wa Ramadhan na wenzetu Wakristo walikuwa kwenye mfungo wa Kwaresma,hii inatuonesha Serikali haina dini ila watu ndio wenye dini zao.Hii inatujenga na kutukumbusha kuwa sisi wote ni wa Mungu,ni kitu kimoja japokuwa kila mtu anaishi kwa imani yake”ameyasema hayo Sheikh Abubakari.
Mkazi wa Same Mjini, Suleiman jumaah amesema matendo mema yana mchango mkubwa katika kuchota baraka kutoka kwa Mungu hivyo yeye ni miongoni mwa watu ambao wamepanga kutembelea vituo vya wasiojiweza na kuwasaidia kile alichojaliwa na Mungu ili kufurahi pamoja nao.
“Matendo mema ni muhimu katika kupata baraka kutoka kwa Allah,hivyo mimi na familia yangu leo tumepanga kutoa sadaka yetu kwa kutembelea kituo Cha wasiojiweza Mjini hapa ili na wao wafurahi kama sisi tunavyofurahia sikukuu hii ya Eid El Fitri”