Aprili 9, 2024 imefunguliwa kesi ya Uhujumu Uchumi ECO. 8641/2024 katika Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mbele ya Mh. Gasper Luoga.
Shauri hili ni la Jamhuri dhidi ya OMARY SALUM HUSSEIN (Aliyekuwa Mtendaji wa Kata ya Ibindi, Halmashauri ya Nsimbo, Wilaya ya Mpanda) na Wenzake watatu ambao ni MUSA BUSWAKALA (Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi – Kata ya Ibindi); OBADIA MAREKANI (Afisa Maendeleo ya Jamii – Kata) na KELVIN MAYANGA (Mjumbe wa Kamati ya Serikali ya Kijiji).
Hati ya Mashtaka imesomwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Kelvin Mwaja, kwamba kwa tarehe tofauti za Mwezi Novemba 2022 Washtakiwa walitumia madaraka vibaya kwa kuuza Gypsum 9 zilizobaki katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Ibindi kinyume na Sheria ya Manunuzi na kujipatia manufaa ya Shilingi 115,000/=.
Washtakiwa wamejihusisha na vitendo vya Rushwa kinyume na k/f cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 marejeo ya Mwaka 2022.
Washtakiwa wamekana makosa. Mshitakiwa wa kwanza yupo nje kwa dhamana na washtakiwa watatu wamekosa dhamana kwa kuwa hawakuwa na wadhamini.