NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
SHEIKH wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke,amehimiza waumini wa Dini ya Kiislamu kuishi kwa upendo,umoja na kudumisha amani ya nchi na kutoa zaka.
Pia wamwombee Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na nchi yetu baraka, wakaboreshe taarifa zao katika daftari la kudumu la wapiga kura wawe na sifa yakupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Sheikh Kabeke ametoa kauli hiyo,leo katika hotuba ya Sala ya Eid El Fitri iliyoswaliwa kimkoa katika Uwanja Nyamagana jijini Mwanza.
Amesema Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umewaunganisha na kuwaweka pamoja waislamu wote,hivyo wajitahidi kuungana na kuwa wamoja bila kujali itikadi zao za kidini katika kudumisha amani,upendo na mshikamano.
“Hatuwezi kupata maendeleo tukiwa tumegawanyika na haifai baada ya Ramadhani turudi kunyoosheana vidole huyu Shia, Ibadhi au Suni,haitusaidii.Tusimame pamoja na tuwaheshimu viongozi wetu na Mwenyezi Mungu hawezi kutuacha,”amesema Sheikh Kabeke.
Amewaasa waislamu wa Mwanza wawe wamoja wasiwe watu wa kutukana ama kwenda kumpiga mwislamu mwenzao kwa kuwa huo ni ukafiri kwa sababu Uislamu ni dini ya amani,hivyo waendelee kumcha Mungu na kutenda mema muda wote.
“Dini yenu ni ya amani,unapokutana na mtu unamtamkia amani (Salaam Aleykum)pia,dini imetuwekea utaratibu wa kukumbuka kutunza amani na Tanzania inasifika kwa hilo.Itakuwa ajabu mwislamu kuvunja amani ambayo hata ndani ya familia tunaitaka na kuna umuhimu wa kuitunza,”amesema Sheikh Kabeke.
Amewasistiza kuishi kwa usalama na jamii mitaani bila kubughudhiana kwa sababu dini yao ni ya amani,asitokee mwislamu akaivunja amani au kutoa lugha na maneno yanayoweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani.
Akizungumzia utoaji zaka misikitini amesema,wapo waislamu ni matajiri lakini hawatoi fungu la kumi la mapato yao (zaka) na kuwataka kutimiza takwa hilo.
“Tunapata majanga sababu ya kutokutoa zaka,zaka haitolewi kwa kujisikia kuwa leo nina elfu 10,nampa masikini la! Ni fungu la kumi la mapato yako na wengine ni wakulima hawatoi zaka ya mazao,pia wachimba madini na wafugaji, tulipeni zaka ni wajibu tumeusahau,”amesema Sheikh Kabeke.
Ameeleza kuwa matatizo yanayowakumba watu wengi yanatokana na kutokutosheka,hivyo tajiri mkubwa ni aliyetosheka katika nafsi yake na kuwataka waislamu waridhike na walichojaliwa,waishi kwa hofu na kumwogopa Mwenyezi Mungu.
Pia waiishi Q’uran kwa kula,kulala,kufanya na kuacha yote yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu huku wakijiandaa kabla ya kuondoka duniani kwani, siku hiyo ikifika hakuna ujanja.
“Mungu hafanyi jambo bila sababu,mtalipwa kwa matendo mliyotenda kwani yeye asema mmefaradhiwa funga.Hivyo usidhani wewe ni wa kwanza,kumbukeni kumcha Mungu maana yake asikukute alipokukataza akukute alipokuagiza,”amesema.
Sheikh huyo wa Mkoa wa Mwanza amewasistiza waislamu kuzingatia mafundisho ya Mwenyezi Mungu,waendelee kumcha na kutenda mema huku akiwaonya wanaotumia vileo na dawa za kulevya aina ya mirungi kuwa imeharamishwa na imewaharibu vijana wengi.
“Ramadhani ilitutengeneza tukaswali tukaacha ulevi tukaacha kutukana.Leo ni siku ya kusaidia yatima waliokosa wazazi wao,wajane na masikini,tuwatafute yatima tuwasaidie.Tujiulize hivi baada ya Ramadhani tutakuwa watu wa namna gani? ” amesema kwa kuhoji.
Kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, mwaka huu,Sheikh Kabeke amewataka waislamu kwenda kuboresha taarifa zao katika daftari za wapiga kura wapate sifa ya kupiga kura.
“Ni mwaka wa uchaguzi wa serikali za mitaa, tuhakikishe amani inadumu,tukahuishe taarifa zetu tuwe na uhalali wakupiga kura.Unayetaka uongozi nenda chama chochote uchukue fomu ya kuomba kugombea.Siku ya kupiga kura tusibaki nyuma tujitokeze kuchagua viongozi tunaowataka,” amesema.
Aidha wasisahau kufanya jambo aliloanzisha Mwenyezi Mungu la kumtakia Rehema Mtume Muhammad S.A.W,waendelee kumheshimu na kumwombea Rais Dk.Samia kwani madaraka hayo amepewa na Mungu amemkubali,hivyo hakuna nafasi ya kumdharau.