Na Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa, Dodoma.
SEKTA ya afya ni miongoni kwa sekta muhimu katika nchi kwani ina mchango mkubwa katika kuwezesha wananchi kutimiza majukumu yao ya kila siku likiwemo jukumu kubwa la ujenzi wa taifa.
Ili wananchi waweze kutimiza kikamilifu jukumu la ujenzi wa taifa lao kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi wanazozifanya, mathalani, shughuli za kilimo, uvuvi, ufugaji, viwanda, biashara, ujasiriamali na kadhalika, ni lazima wananchi wawe na afya njema, ndiyo maana Wizara ya Afya ina msemo usemao “Mtu ni Afya, Jali Afya Yako.”
Mtu anapokosa afya njema, hawezi kuzalisha, atatumia fedha nyingi kujitibu lakini pia ndugu wanaomzunguka watalazimika kuacha shughuli za uzalishaji ili kumuuguza. Kutokana na umuhimu na unyeti wa kipekee wa sekta ya afya, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi shupavu wa Dk. Samia Suluhu Hassan, sekta hii imepatiwa kiasi cha shilingi Trilioni 6.722 kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya katika ngazi zote ili wananchi popote walipo wanufaike na huduma za afya.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia katika sekta ya afya, Waziri Ummy Mwalimu anasema: “Ndani kipindi cha miaka mitatu serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa na bidhaa nyingine za afya, upatikanaji wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi nchini, kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa ikiwemo huduma za mionzi, kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, kudhibiti maambukizi ya HIV/UKIMWI, kifua kikuu, malaria na magonjwa ya mlipuko, ajira kwa watumishi na ufadhili wa wanafunzi katika ngazi za fani mbalimbali pamoja na kupitishwa kwa sheria ya bima ya afya kwa wote.”
Ikumbukwe kuwa miongoni mwa vipaumbele sita vya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2024/2025 ni pamoja na ubora wa huduma za afya inayotolewa kwa wananchi.
Wizara imeweka mkazo na msukumo mkubwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwani pamoja na uboreshaji na ujenzi wa miundombinu bora ya afya iliyopo sasa, kama wananchi hawatapewa huduma bora, miundombinu hiyo haitakuwa na maana kwa wananchi wanaohitaji huduma.
Akizungumza na Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Afya Aprili 4, 2024 lililokutana kwa siku moja jijini Dodoma kwa ajili ya kupitia utekelezaji na ufafanuzi wa hoja mbalimbali pamoja na mikakati ya kutoa huduma bora kwa wananchi sambamba na kujadili bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2023/2024 na 2024/2025, Waziri Ummy Mwalimu alisisitiza wahudumu wa wizara ya afya kuzingatia ubora wa huduma za afya wanazozitoa kwa wananchi kwani ubora wa huduma zao ni agenda muhimu katika wizara hiyo.
Waziri Ummy alisisitiza kuwa serikali inafanya juhudi kubwa kufikisha huduma bora wa kwa wananchi popote walipo. “Tunajua tumefanya vizuri sana kwenye miundombinu na vifaa tiba, lakini tumeendelea kulalamikiwa kwenye eneo la huduma, hususani ngazi ya msingi, huku juu kwenye kanda na ngazi ya hospitali za rufaa za mikoa, tumejitahidi sana.
“Rai yangu kwenu tuendelee kusaidia katika kuimarisha huduma kwenye zahanati, hospitali za wilaya na vituo vya afya. Jambo tukishakubaliana kwenye vikao halali, tunatakiwa kwenda kwenye utekelezaji, tunapoendelea kuzunguka na kupiga danadana tunawakwamisha wananchi na mwisho wa siku tunalaumiwa. Niliombe baraza hili, mnapojadiliana suala hili mlipe kipaumbele.” amesema Waziri Ummy.
Kimsingi, haipendezi uwekezaji mkubwa uliofanyika katika sekta ya afya ukachafuliwa kwa wananchi kuendelea kulalamikia huduma zinazotolewa na wahudumu wa afya hasa katika matumizi ya lugha na kujali muda katika kuwahudumia wananchi.
Pindi mwananchi anapofika kwenye kituo cha kutolea huduma anahitaji kupata faraja kutoka kwa watoa huduma kupitia lugha nzuri, ya staha na ya upole. Huduma bora kwa wateja pekee inaweza kumpa mgonjwa unafuu katika ugonjwa unaomsumbua.
Hivyo basi, ni vyema wananchi wakapokelewa, kusikilizwa, kuhudumiwa na kupata huduma zote muhimu ili mwananchi aone umuhimu wa kwenda kupata huduma za afya kwenye vituo rasmi.
Februari 15, 2024, akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Kisera wa 23 wa Sekta ya Afya uliofanyika jijini Dodoma, Waziri Ummy alisema: “Suala la ubora wa huduma za afya tunaendelea kulisisitiza kwa kuzingatia umuhimu wa kuboresha huduma kwa wateja pamoja na kuhakikisha usalama wao ili mteja apate huduma iliyokuwa nzuri.”
Kwahiyo, kitendo cha Waziri Ummy kuendelea kusisitiza utoaji wa huduma bora kwa wananchi mara kwa mara kila apatapo nafasi ya kuzungumza, kinaonesha ni kwa namna gani amedhamiria kuona wananchi wanapata huduma bora kwani sekta ya afya inawahudumia wananchi moja kwa moja, uso kwa uso kila siku katika ngazi mbalimbali kuanzia kwenye vijijini hadi mijini.
Kama hiyo haitoshi, akiwa mkoani Shinyanga mwezi Julai, 2023 kwenye ziara ya kikazi, Waziri Ummy aliwasisitiza wataalamu wa afya kuboresha zaidi utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia matumizi ya lugha na kauli zenye staha kwa wananchi na kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vipimo ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za afya.
Waziri Ummy alisema: “Ndugu zangu wataalamu wa afya, nipende kuwasisitiza sana katika kuzingatia weledi, maadili, miiko na utu katika utoaji wa huduma kwa wananchi wetu huku tukitumia muda mwingi zaidi kutatua kero na kupunguza malalamiko kwa wananchi wetu na kwa kuhakikisha pia madaktari mnaandika dawa kwa kufuata miongozo ya vitabu vya dawa vya taifa ili kuondoa malalamiko kwa wagonjwa wetu.”
Pengine sasa ni wakati mwafaka kwa wahudumu, watumishi na wataalamu wa afya kubadilika na kuhakikisha wananchi wanaofika kupata huduma wanawahudumia vizuri. Sekta ya afya imebeba uhai wa binadamu, hivyo ni muhimu kuwahudumiwa wananchi vizuri ili waweze kupona na hatimaye kurejea kwenye shughuli zao za uzalishajimali kwa kuwa na afya njema kwa maendeleo yao na ya taifa pia.
Kwangu mimi, sina deni kwa Waziri mwenye dhamana ya afya-Ummy Mwalimu kwani amesisitiza vya kutosha uzingatiaji wa utoaji wa huduma bora za afya kwa wagonjwa, kazi kwenu wataalamu wa afya kutendea kazi maagizo na maelekezo haya. Lakini kubwa kwa watumishi na wataalamu wa afya kuzingatia ni kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi shupavu wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, inataka kuona wagonjwa na wananchi wanahudumiwa vizuri ili kuimarisha afya zao kwa maendeleo yao na ya nchi yao pia.
Dk. Reubeni Lumbagala ni Mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800462