Na Prisca Libaga Arusha
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini imetoa elimu juu ya madhara ya tatizo la dawa za kulevya kwa Maafisa na Wahifadhi Udhibiti Wanyamapori zaidi ya 35 katika Jumuiya ya Uhifadhi wa Wanyamapori ya Enduiment (WMA) iliyopo Kata ya Tingatinga wilayani Longido.
Maafisa na Wahifadhi hao katika shughuli zao za kila siku wakati fulani hukutana na kuwadhibiti wahalifu wanaosafirisha dawa za kulevya hususani mirungi na bangi kupitia vipenyo vya mpakani kwa kutumia njia za panya kuelekea mjini Arusha.
Hivyo, elimu juu ya madhara ya matumizi dawa za kulevya, udhibiti wa usafirishaji haramu wa dawa za kulevya na sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya itakuwa chachu kwa maafisa hao kuimarisha mapambano katika maeneo yote ya hifadhi ili wahalifu wa dawa za kulevya wasiweze kusafirisha dawa za kulevya kupitia maeneo hayo yenye vipenyo.