Mkuu wa wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa.
……………………..
Serikali imeanza mchakato wa kumaliza mgogoro wa ardhi unaoendelea kati ya viongozi wa kimila (Machifu) na Taasisi ya Utafiti ya Kilimo (TARI) katika eneo la chuo cha kilimo Uyole Jijini Mbeya.
Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mhe. Beno Malisa amefikia uamuzi huo baada ya kukutana na pande zote mbili, Machifu na TARI na kusikiliza hoja za pande hizo ambapo machifu wanadai eneo la hekari nane walilotengewa sio eneo sahihi huku wakidai eneo lenye makaburi ya viongozi wao wa kimila waliofariki miaka kadhaa iliyopita ndio eneo sahihi wanalopaswa kukabidhiwa.
Kwa upande wa kituo cha utafiti wa kilimo TARI wanadai kuwa eneo walilowapatia machifu ni eneo sahihi ambalo linawatosha kufanya shughuli zao za kimila ambapo gharama zimetumika kuweka uzio kwa ajili ya kulitambua eneo hilo na kwamba halitotumika kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Aidha Mhe. Malisa ametaka kuundwa kwa kamati itakayojumuisha baadhi ya watu kutoka upande wa machifu na upande wa TARI kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ili kulipatia ufumbuzi suala hilo haraka iwezekanavyo.
Mhe. Malisa amezitaka pande zote mbili kuwa watulivu katika kipndi hiki ambacho ya mgogoro huo unatafutiwa ufumbuzi na kusimamisha shughuli za kimila na kilimo katika eneo hilo mpaka pale ambapo majibu yake yatapatikana siku za hivi karibuni.