Iringa,
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff amemtaka Mkandarasi ambaye ni China Henan International Cooperation (CHICO) kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara za lami za Mtili- Ifwagi (Km 14) na Wenda- Mgama (Km 19) zinazotekelezwa chini ya mradi wa RISE mkoani Iringa.
Ameyasema hayo wakati alipokuwa kwenye ziara ya ukaguzi wa mradi ili kujionea maendeleo ya mradi huo ambapo amemtaka mkandarasi huyo kutimiza mkataba wake kama ulivyopangwa.
Mhandisi Seff amemtaka Mkandarasi CHICO kuongeza kasi zaidi ili kumaliza kazi kwa muda uliopangwa wa mkataba ili wananchi waweze kutumia barabara hizo katika kujiletea maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.
Wakati huohuo akiwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mhandisi Seff alitembelea ujenzi wa barabara ya Sawala-Mkonge-Iyegeya (Km 10) inayojengwa kwa kiwango cha lami kwa kutumia teknolojia mbadala (Ecoroads).
Mradi wa RISE una lengo la kuboresha barabara zenye fursa za kiuchumi hasa maeneo yenye uzalishaji wa mazao ya kilimo na unatekelezwa katika mikoa ya Iringa, Tanga, Geita na Lindi.