Na Takdir Ali. Maelezo.
Wafadhali na watu wenye uwezo wametakiwa kuwekeza zaidi kwa kuanzisha vituo vya mafunzo ya ujasiriamali kwa Watoto wenye ulemavu ili wawaeze kupata elimu na kujiajiri wakati watakapomaliza mafunzo yao.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu wenye ulemavu Salma Haji Saadati mara baada ya Iftari ilioandaliwa na kituo cha Upendo Mwanakwerekwe na utoaji wa nguo za Skukuu kwa ajili ya Watoto Viziwi, hafla ambayo imefanyika Mwanakwerekwe Ijitimai Wilaya ya Magharibi “B”.
Amesema iwapo wafadhili wataweka mikakati madhubuti ya kuanzisha vituo hivyo wataweza kuwasaidia watoto wenye ulemavu ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwapatia elimu sawawatu wenye ulemavu kama watu wengine.
Aidha amesema Serikali imeanzisha Skuli mchanganyiko ili Watoto hao wapate elimu bila ya kubaguliwa ubaguzi na kuweza kuwa wazalendo wa kuijenga nchi yao na kuwa viongozi bora wa sasa hapo baadae.
Hata hivyo amewaomba wazazi na walezi kufuatilia maendeleo ya watoto wao ili kuwakinga na vitendo viovu ikiwemo udhalilishaji sambamba na kuwaomba wanafunzi kuzingatia masomo ili waweze kufanya vizuri katika mitihani yao.
Kwa upande wa Mfadhili wa Iftari hiyo ,Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya ZOI Kassim Suleiman Ushanga ameahidi kuendelea kutoa misaada mbalimbali kwa jamii ikiwemo watu wenye mahitaji maalum na kuwaomba wanachi kuwaunga mkono kwa kupeleka vijana wao katika chuo cha ZOI ili kuweza kupata mafunzo ya lugha na Ujasiriamali.
Nae Msaidizi Mkuu wa kituo cha Upendo, kinachotoa mafunzo ya ujasiriamali kwa watoto viziwi Mwanakwererkwe Saada Hamad Ali amesema kazi ya kufundisha hasa kwa Watoto wenye ulemavu ni ngumu hivyo wanahitaji kuungwa mkono kwa hali na mali ikiwemo kupatiwa Posho kwa Waalimu, Vitendea kazi pamoja na sare kwa Watoto.
Nao baadhi ya Wananchi walioshiriki katika futari hiyo ikiwemo wazazi na walezi wa Watoto Viziwi wa kituo cha Upendo wamesema wamefarajika sana kwa Watoto wao kufanyia futari hiyo na kuahidi kushirikiana ili Watoto wao waweze kupata elimu itakayoweza kuwasaidia katika kuendesha Maisha yao ya kila siku.