*Itahusisha utoaji wa Leseni ya maeneo ya uchimbaji
*Wachimbaji kunufaika na Magari,Vifaa na Mitambo
*Aitaka Menejimenti ya Wizara ya Madini kusimamia utekelezaji wa miradi ya wachimbaji
Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony Mavunde amesema serikali itatekeleza programu ya Mining for a Brighter (MBT) kwa lengo la kuwainua wachimbaji wanawake na vijana.
Mh Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 08 Aprili, 2024 Jijini Dodoma alipokuwa akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyanyakazi wa Wizara na Taasisi zake na kutumia fursa hiyo kuwataka viongozi na watumishi wa Wizara kuwa wabunifu kila wakati wanapotekeleza majukumu yao.
“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuiimarisha wizara ya madini kwa kuitengea fedha za kutekeleza miradi na mipango mbalimbali.
Mpango mahsusi tunao kuja nao sasa ni Kuwaendeleza wachimbaji wakinamama na Vijana Kupitia programu ya Mining for A Brighter Tomorrow(MBT) yenye lengo la kuwapatia leseni za maeneo ya uchimbaji,magari, vifaa na mitambo ya uchimbaji.
Kupitia programu hii itasaidia kuchochea ukuaji wa sekta ya madini,uchumi wa Taifa na kuongeza ajira kwa watanzania.
Tumieni hili Baraza la wafanyakazi kuhakikisha mnakuja na mpango mzuri wa kusimamia utekelezaji wa mipango na miradi chini ya Wizara.
Nawapongeza kwa jitihada za ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali, nina imani kubwa kwa watumishi wa Wizara kuwezesha sekta ya madini kufikia mchango wa asilimia 10 kwenye pato la Taifa ifikapo 2025.”Alisema Mavunde
Awali, akimkaribisha Waziri wa Madini, Mheshimiwa Dkt. Steven Kiruswa, Naibu Waziri wa Madini aliwapongeza watumishi wote wa Wizara kwa namna wanavyoendelea kujitolea kuhakikisha mikakati yote ya kuendeleza sekta ya madini inafanikiwa.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, ndugu Msafiri Mbibo alieleza kwamba Baraza hilo ni utekelezaji wa wajibu wa mwajiri kwa wafanyakazi na kubainisha kuwa mkutano huo umelenga zaidi katika kupitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2023/2024 na mpango wa bajeti ijayo ya mwaka 2024/2025.