Na Sophia Kingimali.
BENKI Kuu ya Tanzania(BoT) imefafanua sababu ya ongezeko la riba ya Benki Kuu kuwa asilimia sita kuwa ni kudhibiti mfumuko wa bei kwa siku za usoni.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo Aprili8, 2024, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi Benki Kuu ya Tanzania(BoT), Dk. Suleiman Missango amesema mwenendo wa uchumi wa dunia ulikuwa unaashiria uwepo wa mfumuko wa bei hivyo ikaona iongeze riba kutoka asilimia 5.5 hadi asilimia sita katika robo ya pili kuanzia Aprili mwaka huu.
Missango amesema kupanda kwa riba hiyo kumezingatia ukuaji wa uchumi kwa maana ya uwepo wa fedha za kutosha katika mzunguko kulingana na malengo yaliyowekwa.
“ Wengi walijua tunakwenda kuweka ukomo wa riba sio kweli, kwa kupandisha riba hiyo maana yake tunapunguza ukwasi katika mzunguko na hivyo kudhibiti mfumuko wa bei kwa siku zijazo.
“ Kupanda kwa riba hiyo kumezingatia ukuaji wa uchumi , maamuzi mengine yatachukuliwa Julai mwanzoni na riba hii ni ya robo ya kwanza ya Aprili, mwaka huu na inaweza kupungua au kuongezeka kwa kadri ya uchambuzi utakavyokuwa,” amesema
Pia amesema Benki Kuu imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na mabenki ili kudhibiti ujazi wa fedha katika mabenki nakwenye mzunguko.
“Tangu Benki Kuu ianzishe mfumo wa riba ya Benki Kuu mwaka huu badala ya mfumo wa zamani wa ujazi wa fedha hali imeendelea kuwa tulivu na mapokeo yamekuwa mazuri kwa wadau,” amesema.
Dk. Missango amesema hali hiyo imetokana na juhudu kubwa ya kutoa elimu kwa wadau katika sekta na imeahidi kuendelea kutoa elimu kwa wanananchi kuweza kufanya uamuzi sahihi katika shughuli za kiuchumi.