Mkurugenzi wa Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation Bi Asma Mwinyi akikabidhi futari kwa makundi ya watu wenye mahitaji maalum huko Dunga Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Mkuu wa Wilaya ya Kati Sadifa Juma Khamis akitoa neno la Shukrani mara baada ya kupokea sadaka kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar PBZ kupitia Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation.(PICHA NA FAUZIA MUSSA-MAELEZO ZANZIBAR)
…………
Na Fauzia Mussa, Maelezo.
Mkuu wa Wilaya ya Kati Sadifa Juma Khamis amesema Serikali inaridhishwa na utendaji wa Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation katika kusaidia watu wenye mahitaji maalum.
Ameyasema hayo mara baada ya kukabidhi sadaka kwa makundi ya watu hao huko Dunga Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja.
Amesema jukumu la kuisaidia jamii sio la Serikali peke yake bali ni kwa kila mwenye uwezo hivyo uwepo wa taasisi hiyo ni kutimiza malengo ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata mahitaji ya lazima.
Amesema Taasisi hiyo imekua mstari wa mbele siku hadi siku katika kustawisha jamii kupitia makundi mbalimbali ndani ya Tanzainia ikiwemo watu wenye mahitaji maalum katika Wilaya hiyo.
Ameeleza kuwa Taasisi hiyo inatekeleza agizo la Mwenyezi Mungu la kuwasaidia wasiojiweza na kuisaidia Serikali katika harakati za kustawisha Jamii.
“Hichi wanachokifanya Asma Mwinyi Foundation ni cha kupongezwa kwani kumewapa furaha wasiojiweza.” Alisema mkuu huyo wa Wilaya.
Kwa upaande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation Bi Asma Mwinyi amesema sadaka hiyo imetolewa Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) kwa ajili ya makundi maalum ili kupata ya matumizi katika siku chache za mwezi mtukufu wa ramadhani zilizobakia pamoja na sikukuu ya Iddi-el-Fitri.
Mapema Bi Asma amewashukuru PBZ kwa kuwa na imani na Taasisi hiyo na kuitumia kama daraja la kuwafikia wenye uhitaji.
Aidha alieleza kuwa Taasisi hiyo imeanzishwa kwa madhumuni ya kuangalia, kuwaenzi na kuwajali watu wenye mahitaji maalum wakiwemo wajane, wazee mayatima na watu wenye ulemavu.
Nao baadhi ya wanufaika wa msaada huo akiwemo Mkali Shaame Mbwana ameshukuru kwa kupatiwa sadaka hiyo na kusema imekuja wakati muafaka kwani itawasaidia katika kipindi cha iddil-fitri.
Kiasi ya wananchi 53 wakiwemo mayatima na wenye mahitaji maalum katika Wilaya ya Kati wamekabidhiwa vitu mbalimbali ikiwemo Unga, Sukari, Mafuta ya kupikia, Mchele, Maharage na fedha taslim.