*Serikali yarusha ndege ya Utafiti ndani na nje ya ukuta kupata kupata viashiria vya mwamba wa madini
*Taarifa za utafiti kusaidia kuwaongoza vizuri wachimbaji
*Atoa tuzo kwa wachimbaji wanaorudisha kwa jamii(CSR)
*Aongoza futari ya pamoja na wachimbaji wadogo
Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amesema serikali itahakikisha inakuja na suluhisho la migogoro baina ya wachimbaji inayojitokeza katika eneo la machimbo ya madini ya Tanzanite ili kuchochea uzalishaji zaidi wa madini hayo ya vito.
Hayo yamesemwa leo Mirerani,Manyara na Waziri Mavunde wakati wa hafla ya kutoa tuzo kwa Wachimbaji waliotekeleza mpango wa wajibu kwa jamii (CSR) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro,Mkoani Manyara.
“Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan imerusha ndege nyuki ndani na nje ya ukuta wa Mirerani kubaini viashiria vya mwamba wa madini hatua ambayo itapelekea wachimbaji wengi kuchimba kwa uhakika.
Kupitia utaratibu huu wa kupata viashiria vya mwamba wa madini itasaidia kutatua changamoto ya mtobozano chini ya ardhi kwa wachimbaji wengi kujikuta eneo moja la uchimbaji na hivyo kupelekea migogoro miongoni mwao.
Ninawapongeza wachimbaji wote mliorudisha kwa jamii kwa kuboresha huduma za Afya na Elimu,niwaombe Halmashauri ya Wilaya kwa kushirikiana na Chama cha Wachimbaji Manyara(MAREMA)kuweka utaratibu mzuri zaidi ili kundi kubwa la wachimbaji liweze kuchangia huduma za msingi kwa jamii”Alisema Mavunde
Akitoa salamu zake,Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mh. Christopher Ole Sendeka ameishukuru Serikali kwa kuendelea na ujenzi wa kituo cha Biashara ya Madini-Tanzanite Exchange Centre(TEC) ambacho kitachochea maendeleo na ukuaji wa kasi wa Mji wa Mirerani.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi,Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mh. Queen Sendiga amewataka wamiliki wa Leseni kuwa mstari wa mbele kuchochea maendeleo ya Jamii zinazonguka machimbo ya madini ili kuboresha huduma za msingi na kukuza uchumi wa Jamii husika.