Kaimu Katibu Msaidizi ,Ofisi ya Rais , Sekretarieti ya ajira katika utumishi wa umma Selemani Sabihi Chihembe akiangalia usaili kwa njia ya mfumo “ONLINE APTITUDE TEST” huko Taasisi ya Karume (KIST) Mbweni Zanzibar.
Baadhi ya vijana wakifanya usaili kwa mara ya kwanza kupitia mfumo “ONLINE APTITUDE TEST” unaolenga kurahisisha zoezi hilo, huko Taasisi ya Karume (KIST) Mbweni Zanzibar.
Afisa Tehama I(CT) Chuo cha Karume Zanzibar Omar akisimamia zoezi la usaili kwa njia ya mfumo “ONLINE APTITUDE TEST” Chuo cha Taasisi ya Karume (KIST) Mbweni Zanzibar (PICHA NA FAUZIA MUSSA –MAELEZO ZANZIBAR)
……..
Na Fauzia Mussa. Maelezo. 07/04/2024.
Kaimu Katibu msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Selemani Sabihi Chihembe amesema ofisi hiyo hiyo imezindua mfumo maalum wa kufanya usaili (ONLINE APTITUDE TEST) ili kurahisisha zoezi hilo.
Akizungumza katika uzinduzi huo ulioambatana na usaili huko Taasisi ya Karume Mbweni Wilaya ya Magharibi “B” amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza gharama za wasailiwa ambao wanatumia masafa marefu kufuata usaili na kutumia muda mwingi kufika katika vituo vya usaili.
“Tumekuwa tukikosa watu wazuri kutokana na watu hao kushindwa kufika eneo la usaili, mtu anaishi Pemba usaili unafanyika Mwanza hana uwezo anaamua tu kuacha ndio tukaona tuanzishe mfumo huu kwa Tanzania nzima ili kila mtu apate hii fursa.” Alieleza kaimu katibu msaidizi huyo.
Amefahamisha kuwa Ofisi hiyo imetenga vituo maalum vyenye miundombinu ya Tehama kwaajili ya kuendesha zoezi hilo na kuwataka vijana kuendelea kuomba nafasi za ajira wakati zinapotangazwa.
“Tupo hapa Karume kwa Mkoa wa Mjini Magharibi, chuo kikuu cha Zanzibar (SUZA) kwa watu wa Mkoa wa Kusini, Chuo cha mafunzo ya Amali Mkokotoni, Mchangamdogo na maeneo mengine mbalimbali.” Alieleza Chihembe.
Kwa upande wake Afisa Tehama Taasisi ya KarumeZanzibar ambae pia ni msimamizi wa usaili huo Omar amesema mfumo huo utaweza kusaidia kuondosha changamato zilizokuwepo ikiwemo kuokoa muda, gharama pamoja na kupunguza idadi ya wasimamizi.
“Hapo awali lazima wawepo wasimamizi zaidi ya 4 katika chumba kimoja lakini kwa mfumo huo sasa utaweza kutumia msimamizi mmoja kwa ajili ya msaada wa dharura endapo utatokezea”. alisema afisa huyo.
Nao baadhi ya Vijana waliofanya usaili wakiwemo Yussuf Ali Mwinjuma na Michel John Warioba wamesema mfumo huo ni rafiki kwani unatoa muongozo wa mambo mbalimbali ikiwemo matumizi ya muda.
Hata hivyo wameishauri Ofisi hiyo kutoa elimu juu ya mfumo huo kwa waombaji ili kuondoa usumbufu wakati wa matumizi na kuweza kufikia malengo yaliokusudiwa.
Uzinduzi wa mfumo wa ONLINE APTTUDE TEST ulizinduliwa rasmi na kuanza kufanyakazi April 06, 2024 katika maeneo mbalimbali ya Tanzania bara na Visiwani.