Mkurugenzi wa Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation Asma Mwinyi akizungumza katika hafla ya futari iliyoandaliwa na Taasisi hiyo kwaajili ya watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali .
Katibu mkuu Wizara ya Maendeleo ya jamii wazee jinsia na watoto Mhe.Abeda Rashid Abdalla akitoa nasaha katika futarisho lililoandaliwa na taasisi ya Asma Mwinyi Foundation kwaajili ya watu wenye ulemavu huko Mazizini Zanzibar.
Sehemu ya washiriki wakiwa wakiwa katika futari iliyondaliwa na Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation huko Mazizini Zanzibar.
(PICHA NA FAUZIA MUSSA- MAELEZO ZANZIBAR)
………….
Na Fauzia Mussa, Maelezo Zanzibar
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Wazee Jinsia na Watoto Abeda Rashid Abdalla amesema Serikali ipo pamoja na Taasisi binafsi zinazounga mkono juhudi za Serikali katika kuisaidia jamii kupata mahitaji mbalimbali.
Akizungumza katika futari maalum iliyoandaliwa na Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation kwaajili ya watu wenye ulemavu huko Mazizini Wilaya ya Magharibi “B” Bi Abeda amesema ili jamii iweze kunufaika zaidi misaada kutoka kwa Taasisi hizo inahitajika.
Aidha amaezitaka taasisi nyengine kuiga mfano huo ili kuweza kuyafariji makundi yenye mahitaji maalum ikiwemo ya watu wenye ulemavu ambayo yanaonekana kusahauliwa.
Mapema alimshukuru na kumpongeza Mkurugenzi wa Taasisi hiyo pamoja na walio nyuma yake ambao wanamsukuma kutekeleza majukumu yake yanayoyagusa moja kwa moja makundi hayo ambayo yanaonekana kuwekwa nyuma.
Bi Abeda amesema kuwa makundi ya watu wenye ulemavu yana uhitaji mkubwa kutokana na hali zao na kumuomba mkurugenzi huyo kuendelelea kuwafiriji na kuwafikia popote walipo ndani ya Zanzibar kwa lengo la kupata radhi za Allah.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation Bi Asma Mwinyi amesema hafla hiyo ni muendelezo wa kuwafikia watu wenye mahitaji maalum ambapo Katika kipindi cha ramadhani Taasisi hiyo imejipanga kulifikia kundi hilo kwa kuwapatia misada mbalimbali pamoja na kujumika nao katika futari.
Bi Asma ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya jamii,jinsia,wazee na watoto kwa mashirikiano yao wakati wote wanapotekeleza majukumu yao kwa jamii.
Hata hivyo aliziomba Taasisi za binafsi na Serikali kushirikiana kwa pamoja kuwakumbuka na kuwajali watu wenye ulemavu kwani nao ni sehemu ya jamii.
Nao washiriki katika futwari hiyo akiwemo Mwenyekiti wa watu wenye ulemavu Magharibi B Hidaya Kisisa wameishukuru Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation kwa kuwaandalia futari hiyo, jambo ambalo limelmewakutanisha pamoja na kuleta faraja ndani yake.
“Tunashukuru sana Kwa hafla hii na sisi tumejiona ni sehemu ya jamii, tunajihisi tunapendwa , kujaliwa na kuthaminiwa ,mungu akupe uwezo uwafutarishe na wenzetu katika maeneo mengine” walisema
Hata hivyo wamemuomba mkurugenzi wa taasisi hiyo kulifanya jambo hilo kuwa endelevu ili kuweza kunufaika na makundi mengine yene uhitaji kama wao.
Jumla ya watu 50 wenye ulemavu wa aina mbali mbali ikiwemo uziwi kutoka Mkoa wa mjini Magharibi wamenufaika na futari hiyo iliyondaliwa na Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation kwa ufadhili Taste me.