DODOMA
Mwananchi Mmoja anejulikana kwa jina la Simon Mkondya ameanzisha kijiji cha Nguruwe katika kitongoji cha Zamahero kijiji cha Mayamaya wilayani Bahi mkoani Dodoma chenye nguruwe zaidi ya 800 na kisha kuvutia maelfu ya watu kutoka ndani na nje ya Tanzania kutembelea kijiji hicho na kuona tamaduni zake.
Mkondya ambae ni muasisi wa kijiji cha Nguruwe ambae pia ni mkurugenzi wa Nguruwe Project amesema katika kipindi cha miezi mitatu kijiji hicho kimepokea watalii wa ndani na nje wapatao 1400 ambapo kutoka mataifa ya Ugaibuni Zamahero kimepokea ugeni kutoka mataifa ya Uholanzi ,Venezuela ,Ujerumani na Ufaransa,Colombia,Ufilipino na China wakitaka kujua sababu iliyomsukuma mfugaji huyo kuanzisha kijiji cha Nguruwe na pia kufahamu tamaduni na changamoto za kuishi na mfugo unaodaiwa kuwa ni mchafu nguruwe.
Akiweka bayana sababu ya kuja na wazo hilo muwekezaji huyo ambae ametoa ajira pia kwa vijana wengi kuhudumia mifugo hiyo na mifugo mingine kama Kanga na Kuku amesema ni kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya kitoweo cha nyama ya nguruwe ambapo anasema utafiti umeonyesha watu zaidi ya bilioni moja kutoka bara la Africa ni walaji wakubwa wa kitoweo hicho na kisha kualika wenye nia ya kuwekeza ufugaji wa nguruwe katika kijiji hicho.
Katika hatua nginyine Mkondya ameweka bayana kwamba katika kijiji hicho kuna aina tatu za nguruwe lakini aina ambayo nyama yake imekuwa ikipendwa na akina dada ni Large White ambayo walaji wanadai inasaidia kuongeza muonekano(shape) kutokana na kuwa na mafuta mengi jambo ambalo limekuwa kinyume kwa akina kaka ambao hawapendelei nyama yenye mafuta kwa kuogopa kunenepa.
Haji Mgogo ni moja ya makumi ya wafanyakazi wa kijiji cha Nguruwe wenye jukumu la kulisha mifugo,Kusafisha mabanda na kutibu pindi inapougua anasema ajira hiyo imemfanya kujenga kibanda chake na kuendesha maisha tofauti na ilivyo kuwa awali alipokuwa hana kazi na kisha kutoa rai kwa vijana kuacha kuchagua kazi.