Wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH) watatoa huduma za tiba mkoba zijulikanazo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services kwa kufanya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa na mikoa ya jirani.
Upimaji huu utafanyika kwa watoto na watu wazima tarehe 15/04/2024 hadi tarehe 19/04/2024 kuanzia saa mbili kamili asubuhi mpaka saa 10 kamili jioni katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa (IRRH).
Kutakuwa na wataalamu wa lishe ambao watatoa elimu ya lishe bora ambayo itawapa wananchi uelewa na kufuata mtindo bora wa maisha utakaowasaidia kuepukana na magonjwa ya moyo ambayo ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na yanaweza kuepukika kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.
Watakaogundulika kuwa na matatizo ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu hapohapo au kupewa rufaa ya kuja kutibiwa katika Taasisi yetu.
Tunawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kupima afya zenu kujua kama mna matatizo ya moyo ili kuanza matibabu mapema kwa atakayegundulika kuwa mgonjwa.