Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Katika kuelekea Siku ya Afya duniani Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro Mhe. Judith Nguli ametoa wito kwa Wakazi wa Wilaya hiyo kuhudhuria katika mabanda ya Wizara ya Afya kupata elimu ya afya, kupima afya .Mhe. Nguli amesema hayo leo April 5, 2024 Ofisini kwake wakati akizungumza na Elimu ya Afya kwa Umma kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani yanayokwenda sambamba na kaulimbiu isemayo “Afya Yangu, Haki Yangu” ambapo Kitaifa yanafanyika Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro tangu April 4 hadi tarehe 7, April, 2024.
Amebainisha kuwa baadhi ya maeneo ya Wilaya hiyo ikiwemo Dakawa na Turiani ni muhimu kuchukua tahadhari.
“Kupitia Maonesho kuelekea Siku ya Afya Duniani, ambapo yanafanyika CCM Kialawa niwasihi wananchi kupitia maonesho hayo tukapate Elimu ya Afya maana Wizara ya Afya imefanya jambo kubwa kutusogezea huduma tena bure”amesema.
Hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya amesema katika kujikinga na Ugonjwa wa Kipindupindu ni muhimu kula vyakula vya moto, kuchemsha maji, kuacha kufungulia majitaka ovyo,kunawa mikono, kuosha matunda kabla ya kula.
Halikadhalika Mkuu huyo wa Wilaya amehimiza umuhimu wa kufuata mtindo bora wa maisha ikiwemo kufanya mazoezi mara kwa mara ,kuzingatia mlo sahihi.