Na WMJJWM, DSM
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Seif Shekalaghe, amekutana na Waziri wa Maendeleo na Afrika kutoka Uingereza Mhe. Andrew Mitchel.
Katika kikao hicho kilichofanyika Machi 04, 2024 jijini Dar Es Salaam viongozi hao wamejadili kuimarisha huduma za ustawi kwa wananchi wanaoishi mazingira hatarishi.
Dkt. Shekalaghe amebainisha baadhi ya jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Wizara nyingine za kisekta pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha upatikanaji wa taarifa sahihi za makundi mbalimbali hasa wahanga wa usafirishaji haramu wa binadamu na watoto waliofanyiwa ukatili zinapatikana.
Aidha, Dkt. Shekalaghe ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa ushirikiano wake katika kuwezesha Tanzania kupitia miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa Mfumo Endelevu wa Kupambana na Rushwa Tanzania – BSAAT ambao utekelezaji wake umefanikisha uundwaji wa kikosi kazi cha kuwalinda watoto dhidi ya usafirishaji haramu wa Binadamu ( AHTCPTF).
Kwa upande wake Waziri wa Uingereza Mhe. Mitshel ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada zake za kuboresha Sera, Sheria na mifumo ya Ulinzi kwa Makundi Maalum na yaliyo katika mazingira hatarishi wakiwemo Watoto na wahanga wa usafirishaji haramu wa binadamu.
Aidha ameahidi kuwa, Uingereza itaendeleza ushirikiano katika jitihada za kuwasaidia wananchi wanaoishi mazingira hatarishi kwa kuimarisha Utekelezaji wa Afua za kikosi kazi maalum cha kupambana na ukatili hususani masuala ya usafirishaji haramu wa binadamu.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera E. Mhando na Maafisa waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.