Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais Hajjat Mhe. Harusi Said Suleiman (wakwanza kushoto) akiwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe.Riziki Pembe Juma , na viongozi wengine katika dua ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan iliyofanyika Kiembesamaki Zanzibar.
……
Na Fauzia Mussa-Maelezo Zanzibar
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk Samia Suluhu Hassan amewataka waislam kudumisha utaratibu wa kuombeana dua ili kuilinda nchi kutokana na majanga mbali mbali ikiwemo mmong’onyoko wa maadili.
Akizungumza kwa niaba yake katika dua maalum ya kumuombea kiongozi huyo huko Kiembesamaki Wilaya ya Magharibi “B”, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Mhe. Hajjat Harous Said Suleiman amesema hatua hiyo itarejesha maadili mema, yanayoonekana kupotea siku hadi siku.
Amesema jamii inakumbwa na vitendo viovu ambavyo vimeathiri mfumo wa maisha uliokuwepo awali na kuisisitiza jamii kusimamia malezi kulingana na muongozo wa dini ikiwemo suala zima la mavazi ili kuwalinda na vitendo vya udhalilishaji.
Akizungumzia kuhusiana na sherehe za sikukuu ya Idilfitri, inayofanyika mara baada ya mfungo wa Mwezi mtukufu wa Ramdahan amewaomba waislam kuhakikisha wanatoa misaada kwa wenzao wasiokuwa na uwezo ili nao waweze kuwa na furaha ya siku hiyo.
Dkt. Samia ameeleza kuridhishwa na juhudi zinazofanywa na Jumuiya mama ya wanawake wa kiislam Zanzibar katika kuwaelekeza Wanawake wenzao misingi bora ya maisha na malezi ya watoto wao pamoja na kuendesha dua kwa viongozi kwa maslahi ya Taifa.
Amesema kitendo cha kuwaombea dua viongozi ni kizuri, cha kupongezwa na kupigiwa mfano kwani kufanikiwa kwa viongozi hao ndio kufanikiwa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Ni vyema kuwaombea viongozi hawa tuliowachagua kwa mapenzi yetu kwani endapo viongozi hao watatereka, watayumba au kuharibikiwa basi ndio tumeharibikiwa wananchi na taifa lote.” Alisema Dkt. Samia.
Baadhi ya wana kamati wa jumuiya mama ya wanawake wa kiislam akiwemo Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Hajjat Abla Sultan na Mratibu wa dua hiyo Zahra Ali Hamad wamesema dua hiyo ni sehemu ya kurejesha shukrani kwa viongozi wa nchi kwa wanavyotekeleza vyema majukumu yao kwa Wananchi.
“Ikiwa huna cha kumlipa mtu kwa wema aliyokufanyia basi muombee Dua” walisema wanakamati hao.
Dua ya kumuombea Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeandaliwa na jumuiya mama ya wanawake wa kiislam Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa, taasisi binafsi na wananchi.