Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri wameongoza mapokezi ya viongozi walioteuliwa na kuapishwa ili kuitumikia Sekta ya Maji hapa nchini, wakiwa pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Maji na watumishi wa wizara hiyo katika Mji wa Serikali Mtumba.
Viongozi waliopokelewa katika ofisi za Wizara, Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ni Naibu Waziri wa Maji Mhe. Kundo Methew (Mb) na Naibu Katibu Mkuu Bi. Agness Meena.
Mara baada ya kupokelewa viongozi hao wameahidi ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha Wizara ya Maji inapiga hatua katika kufikia lengo la Serikali kufikisha huduma ya maji kwa kila Mtanzania, wa mjini na vijijini.
Wamesema wanatambua mahitaji ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji unafika asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025.
“Nimeziona nyuso za furaha kwa watumishi wa wizara. Nina uhakika nitakuwa na furaha katika kazi yangu. Umoja wetu ndio nguzo yetu ambayo itaweza kutufikisha kwenye malengo”. Mhe. Kundo amesema huku Naibu Katibu Mkuu Bi. Meena, akiongeza kuwa wamekuja kufanya kazi baada ya kuaminiwa hawataweza kumuangusha Mhe. Rais Samia katika kufanya kazi. Amesema kuwa anategemea kujifunza mengi kutoka kwa watumishi wa Wizara na yupo tayari kujifunza.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi Mwajuma Waziri kwa pamoja wamewahakikishia ushirikiano na kwamba Wizara ya Maji ina watumishi wenye morali ya kufanya kazi.
Waziri Aweso ameongeza kuwa yapo mafanikio ambayo yamefanyika ndani ya wizara hiyo ikiwemo kuwa kinara kwa miaka miwili mfululizo Duniani katika utekelezaji wa miradi ya maji kupitia program ya Lipa kutokana na matokeo (P for R) na kwamba mafanikio hayo yametokana na utayari wa watumishi wa wizara.
Mhe. Aweso amesisitiza kazi ifanyike zaidi kwa kutumia mifumo ya kisasa ya kidigital ili kurahisisha huduma kwa wadau wote wa Sekta ya Maji. Pamoja na hilo ameainisha kuwa mafanikio yanapatikana kwa kufanya kazi kwa moyo wa ushirikishwaji na kupendana miongoni mwa watumishi na viongozi.