WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imetumia sh. trilioni 10.69 kwa ajili ya ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango cha kimataifa yenye urefu wa kilometa 1,219 kuanzia Dar es Saalam hadi Mwanza.
Akielezea utekelezaji wa miradi nane ya kielelezo kwa mwaka 2023/2024 Bungeni leo (Jumatano, Aprili 3, 2024), Waziri Mkuu amesema hadi kufikia Februari 2024, ujenzi wa reli hiyo umefikia viwango vya kati ya asilimia 5.38 na asilimia 98.84, tayari reli hiyo imeshaanza kufanyiwa majaribio kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro.
“Kama nyote mlivyoshuhudia, majaribio ya treni hiyo ya mwendo kasi yalifanyika kwa mafanikio makubwa mwezi Februari, 2024. Ni matarajio yetu kuwa huduma ya usafiri na usafirishaji itaanza ifikapo Julai, 2024 kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Dodoma,” amesema Waziri Mkuu wakati akiwasilisha Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2023/2024 na Mwelekeo wa Kazi zake kwa mwaka 2024/2025.
Akifafanua kuhusu ujenzi wa reli hiyo, Waziri Mkuu amesema: “Ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (52.69, Makutupora – Tabora (Kilomita 371) umefikia asilimia 13.86, Tabora – Isaka (Kilomita 165) umefikia asilimia 5.38 na Tabora – Kigoma (Kilomita 506) umefikia asilimia 1.81 Kilomita 300) umefikia asilimia 98.84, Morogoro – Makutupora (Kilomita 422) umefikia asilimia 96.35, Mwanza – Isaka (Kilomita 341) umefikia asilimia.”
Akielezea kuhusu mradi wa kuzalisha umeme wa wa Julius Nyerere ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 2,115, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wake umefikia asilimia 96.81 na kwamba kazi zote za mradi huo zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Desemba, 2024.
Amesema zoezi la kuwasha mtambo wa kuzalisha umeme lilifanyika na kufanikiwa kuingiza kwenye Gridi ya Taifa megawati 235 kutoka kwenye mtambo mmoja kati ya mitambo tisa itakayozalisha umeme katika mradi huo.
Kuhusu uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Waziri Mkuu amesema Serikali imekamilisha malipo ya sh. bilioni 753 kwa ajili ya ndege tatu aina ya Boeing 737-9 Max (ndege mbili) na Boeing 787-8 (ndege moja). “Ndege mbili aina ya Boeing 737-9 Max ziliwasili nchini Oktoba, 2023 na Machi, 2024 na nyingine moja inategemewa kuwasili Aprili, 2024 na hivyo kulifanya Shirika hilo liwe na jumla ya ndege 16.”
Akielezea kuhusu mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga lenye urefu wa km. 1,443, Waziri Mkuu amesema Serikali tayari imechangia jumla ya dola za Marekani milioni 268.77 sawa na asilimia 87.27 ya hisa zake.
“Hadi kufikia Machi, 2024 baadhi ya shughuli zilizofanyika ni kukamilisha ulipaji wa sh. bilioni 34.93 zikiwa ni fidia kwa wananchi 9,823 kati ya 9,904 wanaopisha eneo la mradi; kukamilika na kuzinduliwa kwa kiwanda cha kusimika mifumo ya kupasha joto na kuzuia upotevu wa joto kwenye bomba kilichopo Wilaya ya Nzega; na kuanza ujenzi wa matanki manne yenye ujazo wa mapipa 500,000 kila moja ya kuhifadhia mafuta ghafi kabla ya kupakiwa kwenye meli katika eneo la Chongoleani, Tanga.”
Kuhusu mradi wa kiwanda cha sukari Mkulazi, Waziri Mkuu amesema ujenzi wake umefikia asilimia 99 na umegharimu sh. bilioni 320.05 na umetoa fursa za ajira 1,996. “Kiwanda hicho kimeanza uzalishaji tangu Desemba, 2023 na hadi kufikia Machi 2024, tani 1,851 za sukari zimezalishwa na kupelekwa sokoni. Matarajio ya kiwanda ni kuzalisha tani 50,000 kwa mwaka ifikapo mwaka 2026/2027,” ameongeza.
Kuhusu mradi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu wa kilomita 3.2 pamoja na barabara unganishi yenye urefu wa kilomita 1.66 kwa kiwango cha lami, Waziri Mkuu amesema ujenzi wake umefikia asilimia 84.47 na unatarajiwa kukamilika Desemba, mwaka huu. Mradi huu utagharimu sh. bilioni 716.33.
Mradi mwingine ambao Waziri Mkuu ameuelezea ni kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Msalato kilichopo Dodoma ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 54.1 na kwamba hadi kufikia Februari, 2024 zimetumika sh. bilioni 107.64.
Amezitaja kazi zinazoendelea kuwa ni ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, barabara ya viungio, maegesho ya ndege pamoja na usimikaji wa taa za usalama na kuongozea ndege. Ujenzi wa jengo la abiria na majengo mengine utekelezaji umefikia asilimia 17.1.
Kuhusu ujenzi wa meli ya MV. Mwanza “Hapa Kazi Tu”, Waziri Mkuu amesema umefikia asilimia 93 ambapo Serikali imetumia dola za Marekani milioni 44.823 sawa na asilimia 90.87 ya gharama zote za mradi huu ambao unatarajiwa kukamilika Mei, 2024. “Kukamilika kwa mradi huu kutaboresha huduma za usafiri wa abiria na mizigo kwa njia ya meli katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi za jirani za Kenya na Uganda, na kufungua nchi kiuchumi pamoja na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii,” amesema.
Kwa mwaka 2024/2025, Waziri Mkuu ameliomba Bunge liidhinishe sh. 350,988,412,000/- ambapo kati ya fedha hizo, sh. 146,393,990,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 204,594,422,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake.
Pia ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya sh. 181,805,233,000/- kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo sh. 172,124,423,000/- ni za matumizi ya kawaida na sh. 9,680,810,000/- ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.