Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwandeti, John Massawe akizungumza na wanafunzi pamoja na wazazi katika mahafali hayo shuleni hapo.
Afisa Maendeleo ya jamii Arusha DC, Stedvant Kileo akizungumza katika mahafali hayo mkoani Arusha
………
Happy Lazaro, Arusha .
Wazazi wameshauriwa kuwa karibu na watoto wao ili waweze kuzitambua ndoto zao na kuziendeleza badala ya kuwakatisha tamaa kwa kile wanachotaka kufanya kwa maisha yao ya baadaye.
Hayo yamesemwa mkoani Arusha na Afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya Arusha dc ,Stedvant Kileo wakati akizungumza katika mahafali ya 7 ya kidato cha sita ambapo jumla ya wanafunzi 68 walihitimu masomo yao.
Amesema kuwa,kumekuwepo na changamoto kubwa ya wanafunzi kukatishwa ndoto zao na wazazi jambo ambalo linawakatisha tamaa wanafunzi katika kuwa na mwamko wa kuendelea na masomo yao.
“Wanafunzi wengi wamekuwa na ndoto za kuwa watu wakubwa katika maisha ya baadaye lakini wengi wao ndoto hizo hukatishwa na wazazi wao jambo ambalo halitakiwi ni lazima wazazi watambue wajibu wao katika kuwasaidia watoto wao.”amesema .
Mkuu wa shule hiyo ,John Massawe amesema kuwa shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri mfululizo na hiyo ni kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa kati ya walimu na wazazi katika kushirikiana kwa pamoja.
Aidha ametoa onyo kwa wazazi wanaowashawishi watoto wao waseme uongo ili wasiende shule au warudi nyumbani ,kuacha mara moja tabia hiyo kwani kwa kufanya hivyo inakuwa ngumu kwa watoto hao kuwa bize na masomo .
Makamu Mkuu wa shule hiyo ,Lekera Sekai amesema kuwa malengo waliyojiwekea kwa mwaka huu ni kuhakikisha wanafuta kabisa daraja la nne kwa kidato cha nne kwa kuhakikisha wanafunzi wanafaulu wote na kuendelea kuwa shule ya mfano.
Amesema kuwa shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kila mwaka katika matokeo ya kidato cha nne na sita na hiyo ni kutokana na ufundishaji mzuri uliopo shuleni hapo pamoja na walimu bora wanaohakikisha wanafunzi hao wanafikia malengo yao waliyojiwekea.
Aidha Sakei amewaomba wazazi kuhakikisha wanawakumbusha watoto hao wajibu wao wa kujisomea pindi wanapokuwa likizo badala ya kuwaacha wakae wakiangalia tu vitu ambavyo havifai na vinawapotezea muda mwingi.
Naye Afisa elimu taaluma sekondari kutoka Arusha dc ,Prosper Kessy amesema kuwa,amekuwa akisimamia ipasavyo swala zima la elimu kwani katika halmashauri hiyo elimu ndio kipaumbele na kwa kufanya hivyo imesaidia sana kuendelea kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi katika halmashauri hiyo.
Kessy amesema kuwa,halmashauri hiyo imekuwa ikifaulisha kwa asilimia 97.3 na hiyo ni kutokana na ushirikiano wa karibu uliopo katika ya wazazi na walimu kwani wamekuwa wakishirikiana kwa karibu sana katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao mashuleni .
“Nawaomba wazazi watoe ushirikiano wa kuchangia fedha kwa ajili ya uzio wa shule kwani shule wanapokuwa na uzio inasaidia sana kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi na kuondokana na changamoto mbalimbali .”amesema Kessy.