…………………….
*Dkt. Biteko akutana na Mwenyekiti wa Bodi ya EITI ya nchini Norway
*Ushirikiano wa EITI na TEITI kuimariswa
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo tarehe 3 Aprili, 2024 amekutana na kuzungumza na Mwenyekiti wa Asasi ya Bodi ya Kimataifa ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (EITI) ya nchini Norway, Mhe. Helen Clark ambaye ameipongeza Tanzania kwa usimamizi madhubuti wa rasilimali hizo muhimu.
Katika Kikao kilichofanyika kwenye Ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, Dkt. Biteko amesema kuwa, Tanzania inaimarisha usimamizi wa rasilimali hizo ili kufikia viwango vya ubora wa kimataifa pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya EITI na Taasisi inayosimamia Rasilimali hizo nchini (TEITI).
Kwa upande wake Mhe. Clark amesema, ziara hiyo ni hatua muhimu katika kuimarisha usimamizi wa rasilimali hizo hapa nchini ili kufikia viwango vya ubora wa kimataifa unaotakiwa katika usimamizi wa rasilimali pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya EITI na TEITI.
Mbali na majadiliano ya kiserikali, Mhe. Helen Clark pia atakutana na wadau mbalimbali wanaohusika katika sekta hiyo nchini kwa lengo la kujadiliana kuhusu changamoto na fursa za utekelezaji wa kanuni na taratibu za EITI, kujadili njia bora ya pamoja katika kuhamasisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali hizo.
Matarajio ya ziara hiyo ni kuisaidia Tanzania kuimarisha usimamizi bora wa rasilimali zake za madini, mafuta pamoja na gesi asilia sambamba na kuisaidia Tanzania kufikia viwango vya kimataifa katika usimamizi wa uwazi na uwajibikaji na kuendelea kuwa mfano kwa mataifa mengine katika usimamizi wa rasilimali hizo.
Mhe. Helen Clark, amewahi kuwa Waziri Mkuu wa New Zealand, pia amewahi kuhudumu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mipango ya Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).
Kikao hicho kimehudhuriwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Taasisi ya Uhamasishaji Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia Tanzania (TEITI) CPA. Ludovick Utouh, Kaimu Katibu Mtendaji wa TEITI, Mariam Mgaya, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni pamoja na Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda.