Na Sophia Kingimali.
Serikali ya Tanzania na Denmark zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya Elimu,Afya Biashara, Uwekezaji, Nishati pamoja na utunzaji wa mazingira huku Denmark ikieleza utayari wake wa kusitisha nia yake ya kufungua ofisi za ubalozi nchini kufuatia tamko lilotolewa mwaka 2021.
Akizungumza na waandishi wa Habari Leo Aprili 3,2024 jijini Dar es Salaam waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba baada ya kukutana na Waziri wa Denmark anayeshughulikia Ushirikiano wa Maendeleo na Sera ya Hali ya Hewa, Dan Jorgensen aliekuja nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili amesema nchi hizo mbili zimekuwa na ushirikiano wa zaidi ya miaka 50 katika masuala mbalimbali ikiwemo diplomasia.
Amesema ziara ya waziri huyo kutoka Denmark ni ya kwanza tangu nchi hiyo kutoa tamko la kusitisha shughuli zake nchini mwaka 2021.
“Tumekubaliana kushirikiana katika nyanja ya elimu, afya biashara pamoja na kilimo kwani Tanzania itaiunga mkono Denmark katika mpango wao wa kuomba uanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,” amesema Makamba.
Ameeleza kuwa awali nchi ya Denmark ilitangaza kusitisha shughuli zake nchini na kufunga ubalozi mwaka 2021 kisha baadae kutangaza bungeni kusitisha shughuli zake nchini Tanzania kutokana na sababu za kiuchumi tamko ambalo waziri huyo amelitangaza kusitisha baada ya kuridhishwa na hali ya maendeleo ya uongozi bora na demokrasia katika taifa la Tanzania.
Makamba amesema katika mazungumzo yao wamekubaliana kuendeleza ushirikiano na kufanya mambo mazuri ikiwemo kubadilishana ujuzi na uzoefu katika mambo mbalimbali.
Aidha amesema waziri huyo yupo nchi kwenye ziara ya siku mbili ambapo atatembelea maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Denmark anayeshughulikia Ushirikiano wa Maendeleo na Sera ya Hali ya Hewa, Dan Jorgensen amesema nchi ya Dermak itaendelea kushirikiana na tanzania katika nyanja za maendeleo ikiwemo katika kukabilina na mabadiliko ya tabia nchi kutokana na mabadiliko yanayo jitokeza ulimwengu kote.
Amesema wamekuwa na ushirikiano mzuri kati ya nchi hizo mbili katika maeneo mbalimbali na wataendelea kushirikiana kwa malengo hivyo ni fursa kwa nchi hizo.
“Tulikuwa na mazungumzo mazuri na waziri tumekubaliana kushirikiana katika maeneo yafuatayo, elimu, afya, biashara, uwekezaji, nishati na utunzaji wa mazingira na ushirikiano huu umeimarika kutokana na uongozi mzuri wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, ” amesema Jorgensen.