Na Sheha Sheha, Maelezo
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Mhe. Shamata Shaame Khamis amewataka wananchi Kuendeleza amani, upendo na Uzalendo ili kuwaenzi Waasisi wa Mapinduzi.
Akizungumza kwa Niaba yake, Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Ikulu Mhe. Ali Sleiman Ameir Mrembo amesema hayo wakati wa Ziara ya kusoma Dua katika Kaburi la Katibu mkuu wa kwanza wa Chama cha Afro Shirazi, Marehemu Pili Khamis Mpera huko Kisiwandui Mjini Unguja.
Amesema Kiongozi huyo ni miongoni mwa waasisi wa Mapinduzi waliofanya kazi kubwa katika kuleta maendeleo nchini hivyo amewataka Wananchi Kuithamini kumbukumbu yake kwa kudumisha mazuri aliyoyaacha kabla ya kuondoka kwake.
“Yeye ameshaandika kumbukumbu yake, na sisi tunapaswa kuandika kumbukumbu zetu nzuri ambazo zitakuja kurithiwa na wengine”
Aidha, amewahimiza Wananchi kuendelea kufanya mema hapa Duniani ili iwe kinga kwao katika Maisha ya hapa ulimwenguni na kesho akhera.
Nae Katibu Tawala Wilaya ya Mjini Dkt. Said Haji Mrisho amewataka wanafamilia ya Marehemu kuendelea kuwa wamoja na kuyaenzi yale waliyoachiwa na Mzee wao huyo.
Nao wanafamilia wa Marehemu amaeishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana nao na kuwafaraji kutokana na kuondokewa na mzee wao na kuomba kuendelezwa kwa utaratibu huo ili kuenzi mchango wa waasisi hao.
Dua ya kumuombea marehemu Pili Khamis Mpera ni miongoni mwa Wiki ya kuwaenzi Viongozi wa Kitaifa ambapo huanzia tarehe mosi April ya kila mwaka na kilele chake kinatarajiwa kufanyika tarehe 07 April, 2024.