Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameiagiza Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo kuhakikisha inawasimamia, kuwalinda na kutoa elimu kwa wasanii wote nchini kuhusu umuhimu wa kujisajili na kuwa na hati miliki ya kazi zao ili waweze kunufaika na mapato yanayotokana na kazi hizo.
Amesema ni vyema Wizara ikaweka utaratibu rafiki na msisitizo katika masuala muhimu yatakayo wawezesha wasanii kunufaika na fursa zilizowekwa na Serikali ikiwemo mikopo nafuu kwa ajili ya kununua vifaa sambamba na uzalishaji wa kazi za sanaa.
“Wasanii wote tumieni fursa ya uwepo wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Hii ni Wizara kwa ajili yenu, changamkieni kila fursa zinazotolewa kupitia Wizara yenu. Itumieni vema kwani iko kwa ajili ya ustawi na maendeleo yenu.”
Ameyasema hayo jana (Jumapili Machi 31, 2024) alipokuwa mgeni rasmi katika Tamasha la nyimbo za Injili la Mtoko wa Pasaka lililofanyika katika Ukumbi wa The Super Dome Masaki, Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali, imeendelea kuimarisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa kwa lengo la kuwawezesha wasanii kuendeleza kazi zao kwa kuwapa mikopo sambamba na elimu ya ujasiriamali ambapo mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 2.39 imetolewa kwa miradi 113 ya Utamaduni na Sanaa na kuwafikia wasanii 230,685.
“Serikali imetoa mikopo kwa wasanii mbalimbali kununua vifaa vya kisasa vya Studio ili kupunguza adha kwa wasanii kusafiri nje ya nchi kwa ajili ya uzalishaji wa kazi zao.
Aidha, ametoa wito kwa waumini wa madhehebu yote ya dini na Watanzania kwa ujumla, kutumia msimu huu wa sikukuu kuongeza upendo, kudumisha amani na kuhimiza mienendo mizuri kimaadili kwa kuzingatia mila na utamaduni wa kitanzania sambamba na kuyakana matendo maovu ikiwemo ya mauaji, wizi, visasi, wivu, ubakaji, unyanyasaji na ubadhilifu.
“Madhehebu mbalimbali ya dini endeleeni kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha jamii inakuwa na mwenendo mzuri kimaadili na kuzingatia mila na utamaduni wa kitanzania.”
Pia, amewasihi viongozi wa dini na watanzania kwa ujumla kuendelea kumuombea Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili aendelee kuliongoza Taifa kwa mafanikio.
Kwa Upande wake, Waziri wa Sanaa Michezo na Utamaduni Mheshimiwa Damas Ndumbaro amesema Serikali kupitia Wizara hiyo wataendelea kuweka mipango na sera rafiki ili kuwezesha ukuzaji wa vipaji kwa wasanii kuanzia umri wa chini sambamba na kuweka mifumo itakayowawezesha wasanii kunufaika na kazi zao.
Naye, Mkurugenzi wa Wasafi Media ambao ndio waandaaji wa Tamasha hilo Bw. Naseeb Abdul amesema taasisi yake imeweka malengo ya kuwa na Tamasha la Mtoko wa Pasaka kila mwaka ili kuendelea kujenga umoja, upendo na amani miongoni mwa Watanzania.