Na Sophia Kingimali.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sixtus Mapunda ameshauri Chama Cha Wastaafu waliopigana Vita ya pili ya Dunia (TLC) kushirikiana na wakuu wa Wilaya na Mikoa kwenye matawi yao ili kukiimarisha na kutunza historia kwa faida ya kizazi kijacho huku akitoa rai historia hiyo kuwekwa kwenye mfumo wa digital ili iweze kuwafikia watu wengi zaidi.
Hayo ameyasema leo Jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano mkuu wa Chama hicho ambao utachagua viongozi wapya ambapo amesema chama hicho ni muhimu katika kutunza historia ambayo vijana wengi hawaifahamu.
Ameongeza kuwa Wazee 52 waliohai hadi sasa kati ya Wazee 15,000 walioshiriki vita ya pili ya Dunia ni hazina kwa taifa na wenye historia na nchi.
“Tumeambiwa kuwa kwenye vita ya pili ya Dunia mwaka 1939 hadi 1945 ambayo sisi wote hapa tulikuwa hatujazaliwa walienda vitani ni watu 15,000 waliorudi ni takribani 13,000 na hadi sasa waliohai ni 52 na mdogo zaidi ana miaka 100 hivyo ni muhimu kuwaandikia historia kabla hawajafa” Amesema Mapunda.
Hata hivyo ametoa wito kwa waandishi wa habari kuwatafuta Wazee hao waliopigana Vita ya pili ya Dunia na kutengeneza makala ambazo zitawezesha kuweka historia nzuri hususani ya picha ambayo itawasaidia vijana na kizazi kijacho kujua historia ya nchi yao.
Sambamba na hayo amewataka kuhakikisha kuwa wanafanya uchaguzi mzuri wa viongozi ambao utaendelea kukiimarisha chama na kuendeleza urithi kwa kizazi cha wzee hao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TLC Hamis Kwizombe amesema kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo na Wazee hao ni serikali kutowatambua na wanaotambulika ni miaka 50 hadi 70.
Aidha ameiomba serikali kuwasimamia katika kutunza Wazee hao kwani ndio waliobakia na ni tunu ya taifa ambayo imewakutanisha na inayofanya watu wengi kukimbilia Tanzania kama kisiwa Cha amani waliyoipigania Wazee hao.
Amesema lengo la mkutano huo ni kufanya uchaguzi Mkuu wa viongozi wa Chama hicho ambao unahisisha wanachama wa aina nne ambao ni Wazee waliopigana Vita ya pili ya Dunia, Ndugu wa Wazee hao, Wanachama wa heshima na Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais wa Nchi.
Naye Katibu Mkuu wa Chama hicho Charles Lubara amesema malengo ya chama ni kuhifadhi historia ya Wazee kwa faida ya kizazi kilichopo na kijacho.
Amesema tayari wamewasiliana na Wizara ya Maliasili ambapo wamepewa eneo Dodoma ambalo watajenga makumbusho itakayotumiwa na watu mbalimbali kwenda kujifunza historia ya nchi yao.
Nae mmoja ya waliopigana vita hiyo mzee ambaye sasa ana umri wa miaka 103 Mzee Muhando Shangali ametoa rai kwa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuweza kuwafikilia hata kuwapa chochote kila mwisho wa mwezi ili waweze kujihudumia.