PEMBA, 29 MARCH 2024
MKE wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation, Mama Mariam Mwinyi ameitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuandaa muongozo wa kutoa elimu ya hedhi Salama kwenye skuli zote za Msingi na Sekondari za Unguja na Pemba.
Mama Mariam aliyasema hayo kwenye hafla ya ugawaji wa taula za kike kwa wanafunzi wa Skuli mbalimbali za msingi na sekondari huko Jadida, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, hafla iliyohudhuruwa na viongozi mbilimbili kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na taasisi nyengine za umma na Binafsi.
Amesema wanafunzi wamekua wakipitia wakati mgumu kwa kukosa baadhi ya vipindi vya masomo na kuchangia kushuka wa viwango vya ufaulu.
Aidha Mama Mariam Mwinyi alielezea suala la hedhi salama limekuwa changamoto kwa kukosekana uelewa sahihi kwa watoto wa kike na jamii hivyo ameitaka Wizara ya Elimu kuweka mikakati madhubuti na kuongeza uelewa kwa jamii.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar Leila Mohd Mussa alisema, Serikali ya Mapinduzi imekua ikichukua juhudi mbalimbali juu ya suala la hedhi salama lakini bado kuna changamoto ya uelewa mdogo kwa jamii hasa kwa baadhi ya wazazi kushindwa kuwaeleza watoto wao njia salama za kujihifadhi wapokuwa kwenye kipindi hicho.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation, (ZMBF), Fatma Fungo amesema ugawaji wa taula hizo kwa wanafunzi wakike utawasaidia kupunguza usumbufu wanaopitia wanafunzi wa kike wanapokuwa mwenye mizunguko ya hedhi zao.
Alisema taulo hizo zitawasaidia kuwa kwenye hedhi salama na kuwasaidia kutimiza ndoto zao hasa wanapokuwa katika ada zao za mwezi.
Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF), mbali na shughuli nyingi zinazofanywa na taasisi hiyo, ikiwemo kupiga vita udhalilishaji, masuala ya wanawake, vijana na watoto pia inaendeleza kampeni yake ya “Mariam Mwinyi Walkathon” ambayo imewagusa wananchi wengi na kuwafuata walipo ili uchunguza afya zao na kufanya matibabu.
Kampeni hiyo yenye lengo la kuimarisha Afya za wananchi na kutekeleza mikakati ya, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia kampeni ya “Afya bora, Maisha bora” inayowafikishia huduma bora za matibabu wananchi wake. (IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR)