Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya kuhifadhi Qur-an kutoka Ofisi ya mufti Shekh Mziwanda Ngwali Ahmed akitoa taarifa ya mashindano hayo yatakayofanyika kesho April 30 katika viwanja vya N¹ew Amaan Complex
………….
Na Rahma Khamis Maelezo
Zaidi ya nchi saba zitashiriki katika mashindano ya kuhifadhi Qurani Afrika mashariki hapo kesho yatakayofanika viwanja vya New Amani Compelex ikiwemo Mwenyeji Zanzibar.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na mashindano hayo huko Uwanja wa New Amani Complex Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar Shekh Mziwanda Ngwali Ahmed amesema tayari washiki wote wanaotoka nje ya Tanzania wameshafika Zanzibar kushiriki mashindano hayo.
Ameeleza kuwa Zanzibar si mara ya kwanza kuandaa mashindano kama hayo lakini kwa mwaka huu mashindano hayo ni a saina yake kwani yameshirikisha nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Kenya, Uganda, Tanzania Bara Comoro DRC, Kongo na Zambia .
Sheikh Mziwanda amesema kuwa washiriki wa mashindano hayo ya Kimataifa ni wanaume wenye umri kati ya miaka kumi na tatu hadi 23.
Hata hivyo amefahamisha kuwa utaratibu maalumu wa kila mwananchi kufika na kushuhudia mashindano hayo umeshandaliwa na kuwaomba wananchi kutumia fursa hiyo kushuhudia mashindano hayo ili kuhamasika zaidi kuisoma Qur-an na kupata radhi za Alahh (Sw)
“Kila muislamu anapaswa kufika na kuangalia mashindano haya kwani yatawasaidia katika usomaji wa Quran ambayo inasomwa na vijana kwa umakini mkubwa” alifafanua Shekh Mziwanda.
Nae Mkurugenzi wa Habari na Matukio wa Shirika la Utangazaji ZBC Salum Ramadhan amesema kufanyika kwa mashindano hayo ni jambo la kiimani hivyo amewataka wananchi kufika kwa wingi ili kupata radhi za Allah (SW) .
Aidha amewashukuru wadhamini wa mashindano hayo kwa udhamini wao kwani wamefanikisha kwa kiasi kikubwa maandalizi hayo hadi kufikia kilele chake hapo kesho.
Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kuingia uwanjani katika mashindano hayo Mkurugenzi Salum amefahamisha kuwa wanawake wataingilialango namba tatu ,nne na tano ambapo wanaume wataingilia lango namba moja na mbili ili kuepusha mchanganiko kutokana na jambo lenyewe lilivyo na kusema kwamba huduma zote muhimu zitapatikana uwanjani hapo.
Kwa upande wake Meneja wa Masoko na Biashara kutoka PBZ Seif Suleiman Muhammed amesema kuwa jambo hilo litaleta thamani kubwa kwa waislamu kwani kuisoma Quran ni kitu kikubwa hasa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Mashindano hayo yameandaliwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti Zanzibar chini ya udhamini mkuu wa PBZ Bank (PBZ IKHLAS).