Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi,wanafunzi wa shule ya Msingi Jeshini katika Manispaa ya Ilemela,kwa pamoja wakipanda mti shuleni hapo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Twiga wa Kijani.
Wanafunzi wa shule ya Msingi Jeshini, wakinawishwa na Waziri wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira,Dkt.Selemani Jafo baada ya kupanda mti wakishirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela,Ummy Wayayu (aliyeiga magoti nyuma yao).
Mkuu wa Wilaya ya Sengerema,Senyi Ngaga na wanafunzi wa shule ya msingi Jeshini,kwa pamoja wakipanda mti katika hafla ya kuzindua mradi wa Twiga wa Kijani shuleni hapo, leo unaolenga kupanda miti 6,000 nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo (wa tano kutoka kulia),leo akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa ATCL na walimu wa shule ya msingi Jeshini baada ya kuzindua kampeni ya Twiga wa Kijani.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Wezesha Binti na Mama Mjasiriamali (WBN),Latifa Mohamed,leo akizungumza na viongozi mbalimbali, walimu na wanafunzi wa shule ya msingi Jeshini,baada ya uzinduzi wa Mradi wa Twiga wa Kijani unaohusisha zoezi la upandaji wa miti katika shule za 60 za mikoa sita ya Tanzania bara.
Kwaya ya wanafunzi wa shule ya msingi Jeshini, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,wakiimba wimbo wa kutunza mazingira, leo wakati wa hafla ya kuzindua mradi wa Twiga wa Kijani shuleni hapo (Picha zote na Baltazar Mashaka)
…………….
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira,Selemani Jafo ameziagiza halmashauri zote nchini kupanda miti na maua pembezoni mwa barabara ili kupendezesha miji na kutunza mazingira.
Ameagiza leo wakati akizindua kampeni ya Twiga wa Kijani katika Shule ye Msingi Jeshini,wilayani Ilemela inayolenga kupata miti 6,000 katika shule 30 za msingi na sekondari 30 akisema itahamasisha wananchi kutunza mazingira.
Waziri huyo wa Muungano na Mazingira,amesema agenda ya usafi haipendezi kuona jiji au manispaa,uchafu umetapaa katika mitaro,mvua zikinyesha inaziba na kusababisha miundombinu kuharibika,hivyo halmashauri zote zihakikishe zinazipatia zabuni kampuni zenye uwezo wa kukusanya na kuondosha taka miji iwe safi.
“Miji inatia aibu, uchafu umetapakaa,mitaro ya maji inaziba sababu ya uchafu na miundombinu inaharibika. Halmashauri kwa nini hamfanyi beutification katika maeneo yenu? Hakikisheni mnapanda miti mizuri ya kupendezesha na kuvutia miji pembeni mwa barabara ili wageni wakifika waone madhari ya miji yetu,”amesema Jafo.
Pia,kutokana na taifa kukabiliana mabadiliko ya tabianchi,ukame na mvua zisizo na mpangilio,agenda ya kutunza mazingira haina mjadala na kuyataka makampuni na taasisi kupanda miti na kutunza mazingira ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.
Jafo amesema elimu ya mazingira iko chini,shirika la Wezesha Binti na Mama Mjasiriamali (WBM)kujitosa kupandikiza agenda hiyo kwa watoto kupanda miti shuleni,wakipata elimu hiyo itasaidia kutunza mazingira na mradi huo wa Twiga wa Kijani haukuja bahati mbaya.
“Sasa kazi imeanza,nawapongeza ATC (Shirika la Ndege Tanzania) na WBM,kwa kumuunga mkono Rais Dk.Samia kutunza mazingira ambacho ni kipaumbele chake na amekuwa kinara wa mazingira nchini,Afrika na duniani,”amesema Jafo na kuongeza;
“Kupanda miti 6,000 si kidogo,kutachagiza na kuhamasisha jamii kupanda miti kuokoa na kurejesha inayopotea.WBM na TFS shirikianeni kuanzisha vitalu vya miti shuleni visaidie wananchi wa maeneo jirani,halmashauri zitenge bajeti ya kustawisha miche zipande miti milioni 1.5 kwa mwaka,zikifanya hivyo tutafika mahali sahihi.”
Amesema makampuni mengi yanazalisha hewa ukaa na kusababisha athari za mazingira yaige mfano wa ATCL na kuzitaka kampuni zinazozalisha nishati safi ya kupikia kuunga mkono juhudi za serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo kwa jamii kuachana na kuni na mkaa ili kuokoa miti inayokatwa.
Naye mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya Sengerema,Senyi Ngaga,amesema kutokana na kwa idadi kubwa ya watu mkoani humu na ukuaji wake kiuchumi kutunza mazingira ni muhimu.
Amesema mazingira yasipotunzwa tutahatarisha uhai wetu na viumbe vingine,ni muhimu kupanda miti ili kuunga mkono juhudi za Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikali kwa ujumla licha ya changamoto ya kubadili mitizamo ya watu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL,Ladislaus Matindi amesema,usafiri wa anga unachangia uchafuzi wa mazingira kwa kuzalisha hewa ukaa kwa asilimia 2.4 hadi 2.5 na takwimu zinaonesha ifikapo mwaka 2050 kiwango cha jotogesi na uharibifu wa mazingira kidunia kitafikia asilimia tano.
Amesema kuepuka kuongeza uchafuzi na kusaidia sekta binafsi kupunguza hewa ukaa katika anga letu na kuhakikisha hawaongezi uchafuzi wamekubaliana na Jumuiya ya Usafiri wa Anga kutumia injini (Smart) zinazotumia nishati mbadala ya nafaka ( mahindi na jamii ya maharage),badala ya petrol.
Pia,kuhakikisha ndege hazichangii uharibifu wa mazingira kwa kuzalisha hewa ukaa,watapunguza muda wa ndege kukaa angani na kuboresha njia maalumu ili kupunguza gesijoto inayosababishwa na moshi unatokana an kuungua kwa mafuta ya petroli.
Awali Mkurugenzi wa WBM,Latifa Mohamed amesema kampeni hiyo itapunguza athari za mazingira na kuleta maendeleo chanya na endelevu kwa jamii,katika kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kuwawezesha wanawake na mabinti kuondokana na changamoto hiyo na kujiingizia kipato.
Ameishukuru ATCL kuwaunga mkono WBM na jitihada za Rais Dk. Samia za kutunza mazingira zinazokwenda sambamba na malengo ya kampeni ya Twiga wa Kijani kupanda miti 6,000 katika kupunguza athari za mazingira na kuleta maendeleo endelevu kwa jamii.