Na Sophia Kingimali.
Umoja wa wanawake nchini(UWT) umedhamiria kwa vitendo kutekeleza dhamira ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua kuni mwanamke kichwani kwa kuhakikisha inazalisha nishati mbadala kwa ajili ya kupikia.
Hayo yamesemwa leo March 28,2024 Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa UWT Joketi Mwegelo wakati akipokea ugeni wa wawekezaji kutoka china katika jimbo la Changzho walioletwa nchini na kampuni ya Amec Group kwa kushirikiana na Canopus Energy Solution lengo likiwa kujadiliana na kuangalia wanaweza kushirikiana kwenye maeneo gani katika uwekezaji.
Amesema ugeni huo umekuja kwa wakati muafaka kwani Chama Cha Mapinduzi CCM kimetoa maelekezo kwa jumuiya zake kuweza kujitegemea kiuchumi.
“Chama kilitoa maelekezo kwa Jumuiya zake kuweza kujitegemea hivyo sisi kama UWT tumekuwa tukikimbizana ili kuhakikisha tunapata wawekezaji ili kuendeleza maeneo yetu nchi nzima”,Amesema Mwegelo.
Amesema UWT wanampango wa kuzalisha mkaa mbadala unaotokana na mavumbi ya maakaa ya mawe hivyo kutokana na wawekezaji hao kujikita zaidi kwenye teknolojia itawasaidia kutumia teknolijia hiyo katika uzalishaji.
Amesema katika miradi yote watahakikisha wanajielekeza katika kumuwezesha mwanamke hivyo chochote watakachoanzisha kitamgusa mwanamke moja kwa moja ili kuhakikisha wanamuinua kiuchumi.
“Tunajivunia kuwa na kundi kubwa la wanawake hivyo tunauwezo wa kuwafikia wanawake wote nchini hivyo tukijua hawa wawekezaji watakuja kuwekeza kwenye maeneo gani tutahakikisha tunawafikia wanawake husika kwani”,Amesema.
Sambamba na hayo Mwegelo ametoa rai kwa wanawake nchini kuungana,kuwezeshana na kujengana kiuchumi kwani kwa kufanya hivyo wanaweza kufanya mambo makubwa katika uchumi wao na Taifa kwa jumla.
Ameongeza kuwa kwa sasa wapo kwenye usajili wa wanawake kote nchini kwenye mfumo wao hivyo hiyo itawasaidia kuendelea kuwaunganisha wanawake ili hata sera za nchi zilizowekwa ziweze kuwasaidia.
Kwa upande wake Mhandisi Anna Nyangasiwa Kampuni ya Canopus Energy Solutions amesema wawekezaji hao wamevutiwa na mpango wa UWT wa matumizi ya nishati mbadala hivyo watakapo kuja kwa ajili ya uwekezaji watajikita katika matumizi ya nishati mbadala kwa kutumia teknolojia ili kusapoti jitihada za Rais Dkt Samia Suluhu.