Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta (wanne kulia), akiagana na Balozi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Sherif Abdelhamid mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao yaliyohusisha mashirikiano katika sekta ya miundombinu ya barabara na madaraja yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri, Sherif Abdelhamid (kulia) akisisitiza jambo kwenye mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta (wapili kushoto), wakati walipofanya mazungumzo yaliyohusisha mashirikiano katika sekta ya miundombinu ya barabara na madaraja yaliyofanyika jana jijini Dar es Salaam.
………….
Misri wavutiwa na miradi ya PPP ya TANROADS Dar es Salaam27 Machi, 2024BALOZI wa Misri nchini Tanzania, Sherif Abdelhamid amevutiwa na miradi itayojengwa kwa ubia wa kati ya sekta binafsi na umma (PPP) itakayokuwa chini ya Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imeelezwa.
Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta amesema hayo jana mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo na Balozi huyo yaliyofanyika Makao Makuu ya TANROADS jijini Dar es Salaam.
Mha. Besta amesema Balozi huyo ameahidi kushiriki fursa zinazopatikana kwenye miradi ya TANROADS na ameonesha dhamira ya makampuni ya Misri kuja kushiriki kwenye miradi ya PPP, ikiwemo ya barabara ya kulipia ya kutoka Kibaha, Chalinze hadi Morogoro; na Barabara za Mzunguko za Jiji la Dar es Salaam (Dar es Salaam Outer Ring Roads).
Miradi mingine ya PPP ni Daraja la Pili la Kigamboni; Barabara ya kulipia ya kutoka Morogoro hadi Dodoma na barabara ya kutoka Igawa hadi Tunduma.
“Kama alivyosema hizi ni mojawapo ya fursa na uzoefu wa Kimataifa unaonesha kuwa kuna Serikali nyingi Duniani zimefanikiwa kukuza uchumi wao baada ya kushirikisha Sekta Binafsi katika kuboresha baadhi ya huduma muhimu za kijamii zilizopaswa kutolewa na Serikali kwa mikataba maalum, na mfano mzuri ni nchi hizo ni Vietnam, » amesema Mha. Besta.
Mha. Besta amesema pia katika mazungumzo yao wameweza kuainisha maeneo ya mashirikiano katika kuendeleza sekta ya ujenzi na utaalamu wa miundombinu ya barabara na madaraja nchini.
Amesema wamekubaliana ni namna gani Misri wanaweza kushiriki katika kuwajengea uwezo watalaam wa TANROADS kwa kutoa mafunzo maalum na kukubali washiriki kwenda kutembelea Misri kwa ajili ya kujifunza zaidi kutokana na maendeleo waliyoyapata.
‘ »Tunashukuru pamoja na mazungumzo kuwa mafupi yenye lengo la kufahamiana na kujenga mashirikiano, wenzetu wa Misri watakuja tena kuangalia soko la ujengaji wa miundombinu ya barabara » ‘ amesema Mha. Besta.
Pia amesema Balozi Abdelhamid amefurahishwa na ujenzi wa bwawa la Umeme la Mwl Nyerere, ambalo linajengwa na Kampuni ya Arabs Contractors ya kutoka Misri.