Na Dk. Reubeni Lumbagala, Kongwa, Dodoma.
“TUNAFANYA haya katika kusaidia wananchi kero zao mbalimbali ili tutakapo kufa watu wasitutafute kwenye makaburi yaliyonakshiwa na marumaru bali kwenye mioyo ya wale ambao walinufaika na sisi kutokana na haya tunayoyafanya.”Maneno hayo maarufu yaliwahi kusemwa na mfanyabiashara na kiongozi mashauri wa zamani wa Morocco, Abu Abdullah Muhammad Ibn Battutah. Hii kwa mbali inafanana na kauli aliyoitoa wakati fulani Rais wa Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi kwamba ‘Maisha ni historia tu. Basi jitahidi uwe historia nzuri.”
Swali kwa wewe kiongozi katika ofisi ya umma, unadhani kutokana na utumishi wako, hata kabla hujaondoka duniani utakuwa historia nzuri? Utagusa mioyo ya watu watakaokuwa wanakumbuka utumishi wako uliotukuka? Chama cha TANU (Tanganyika African National Union) kilichofanya kazi kubwa ya kuleta ukombozi Tanganyika (sasa Tanzania Bara) kiliweka ahadi zake ambazo wanachama na viongozi wake wa wakati huo na sasa CCM wanapaswa kuzielewa, kuziishi na kuzitendea. Mathalani, moja ya ahadi za za mwanachama wake ni ile isemayo “Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.”
Kimsingi, ahadi hii ina lengo la kuwakumbusha watumishi, watendaji na viongozi kuwa nafasi walizonazo si mali yao, wala si nafasi ya kudumu, bali ni nafasi za utumishi wa umma kwa muda tu na hivyo wanawajibika kuwatumikia wananchi kutoka na kupewa dhamana hiyo na kamwe wasitumie nafasi zao au za watu wengine kwa manufaa yao binafsi.
Licha ya kuwa ahadi hii ni ya wanachama wa CCM, lakini ni ahadi ambayo inapaswa kufanyiwa kazi aliyekabidhiwa ofisi ya umma. Kwa mtumishi au kiongozi anayeelewa vyema ahadi hii na kuifanyia kazi kikamilifu, utumishi wake utaleta manufaa na faida nyingi kwa wananchi na taifa na daima atakumbukwa na kizazi cha sasa na kijacho.
Kuiishi ahadi hii ni kuwatumikia wananchi kwa kuhakikisha maslahi na haki zao wanazipata kwa wakati na kamwe hatakuwa sehemu ya kukwamisha na kuzuia kabisa haki kupatikana bali kuiwezesha kupatikana.
Juzi nilimsikia Sheikh mmoja akiwaambiwa waumini wa dini ya Kiislamu ambao wanaendelea na Mfungo wa Ramadhani kuhusu Hadithi ya Mtume Muhammad (SAW) inayosema kwamba muumini anayemfurahisha sana Mwenyezi Mungu ni yule ambaye watu wengi wananufaika naye. Kwamba kadri unavyopendwa na Mungu kutokana na watu wengi wanavyonufaika na wewe, ndivyo pia Mungui anavyozidi kukupa baraka za hapa duniani na kesho akhera.
Nimpongeze Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ambaye mara kwa mara amekuwa akisisitiza uwajibikaji, uzalendo na moyo wa dhati wa kuwatumikia wananchi kwani kwa kufanya hivyo, kero za wananchi zinatatuliwa na hatimaye ufikiwaji wa mipango na malengo ya nchi unatimia kwa wakati. Mathalani, hivi karibuni Dk. Biteko alifungua Mkutano wa Tano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Nishati, alisisitiza kuwa cheo ni dhamana, hivyo watumishi wa Wizara ya Nishati wakiwemo Tanesco wawahudumie wananchi ili nchi iweze kusonga mbele kimaendeleo.
“Yani wewe kuwa mtu wa Tanesco au kuwa mtu wa Wizara ya Nishati unaonaje fahari kuabudiwa na kutukuzwa kwa sababu ya cheo ambacho kwanza sio chako ni cha watu… Hivi vyeo vyote mlivyonavyo kikiwemo cha kwangu sio vya kwetu ni temporary (vya muda mfupi) kwa ajili ya ku-service (kuhudumia) wakati ule. Kwa nini msijifanyie marafiki kwa vyeo mlivyo navyo? Kwa nini mnajitengenezea maadui kwa vyeo mlivyonavyo? Unafanya Tanesco ambalo ni shirika zuri la nchi linaonekana ni shirika ambalo ni baya la hovyo. Akisimama mtu wa Tanesco mahali popote watu wanaanza kucheka utafikiri kasimama comedian (mchekeshaji), kwa nini? Ni kwa sababu ya character (tabia) za watu wa mle ndani. “Kumpelekea mtu nguzo mpaka akupe hela, na wananchi wapo wanaojua kushawishi. Atakushawishi kwa haraka zake anakwambia, bwana nisaidie niwekee nguzo hapa haraka kuna milioni hapa. Siku nguzo imesimama atakumbuka milioni yake na atakwenda kwa wengine kuwaambia wale jamaa hawapeleki nguzo mpaka milioni, unahangaika hapa, mimi nilivyomgonga milioni, mbona kesho yake ilifika. Tunaonekana wote humu wapiga dili,” alisema.
Kwa viongozi wote wawe wa kuchaguliwa au kuteuliwa wana jukumu la kuwatumikia wananchi wanaowaongoza na kuhakikisha nafasi walizonazo zinakuwa ni daraja la kufanikisha maendeleo badala ya kukwamisha. Wapo wanaoelewa vyema dhana ya cheo ni dhamana na hivyo kwa wakati walionao wa kuwatumikia wananchi wanatimiza wajibu wao kikamilifu na kwa moyo wa uwajibikaji na uzalendo mkubwa. Cheo ni kama koti la kuazima, ambalo kwa kuwa umeliazima ni lazima utalirudisha kwa wenyewe. Ni muhimu kuwa mnyenyekevu katika kuwatumikia wananchi.
Lakini pia wapo baadhi watu ambao kwao cheo ni fimbo ya kuwachapa wengine, na hivyo kutaka kuonesha umuhimu wa nafasi zao kwa kuwakwamisha wengine. Viongozi wanaotumia nafasi zao kuwaumiza wengine, wanapaswa kubadilika kwani cheo ni dhamana. Vilevile, kwa watumishi wa umma waliopewa dhamana ya kuwatumikia wananchi wapo wanaowajibika na wapo wanaokwamisha wengine kwa nafasi walizonazo.
Ninaandika makala haya ili kuwakumbusha wenye vyeo na madaraka katika ofisi za umma kuzingatia kila mara kwamba cheo walicho nacho, ofisi ya umma wanayoitumikia ni dhamana.
Wajue kwamba mshahara wanaolipwa, kiyoyozi wanachofurahia au kama kuna gari wamepewa basi vyote vinatokana na kodi za wananchi wanaovuja jasho ili wao wawatumikie.
Kwamba kimsingi waajiri wao halisi ni hawa wananchi na hivyo si watu wa kusukumwasukumwa bali wanatakiwa wawatumikie. Kwa lugha nyingine walioko kwenye ofisi za umma wajue kwamba ndio watumwa wa wananchi na si kufikiri kwamba wananchi wanapaswa kuwatumikia wao.
Biteko alipokuwa Waziri wa Madini, aliwakumbusha wakurugenzi ndani ya wizara hiyo kuacha ushamba wa kuwanyima magari watumishi wao wa ngazi za chini pindi wanapokuwa na ziara za kikazi kwa kutaka magari hayo wayatumie wao wenyewe hata kama kwa wakati huo hayana kazi ya msingi, kwani kufanya hivyo kunakwamisha maendeleo.
Nimalizie kwa kurudia kuwakumbusha wote waliopewa nafasi mbalimbali za kuwahudumia wananchi kuzingatia kuwa cheo ni dhamana tu, leo wapo kwenye nafasi hizo, kesho wataondoka wengine wataingia. Wananchi wanataka huduma, waliopewa dhamana ya kuwahudumia watimize wajibu wao kikamilifu kwa maslahi na maendeleo ya nchi yetu. Ikumbukwe kuwa huduma bora kwa wananchi ni moja ya mkazo mkubwa unaohimizwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Dk. Samia Suluhu Hassan.
Asante sana Dk, Biteko kwa kuhimiza uwajibikaji na dhana ya cheo ni dhamana. Ukipewa ofisi ya umma, ukipewa cheo, ukichaguliwa kuwa mbunge, ukisoma hadi kuwa profesa usidhani kwamba wewe una uwezo, maarifa na akili nyingi kuliko Watanzania wengine, la hasha. Wapo Watanzania wanaoweza kufanya kazi hiyo ila kwa sasa Mungu amekuchagua wewe. Acha kiburi, tumikia watu ili uwe hadithi nzuri.
Mwandishi ni mwalimu wa Shule ya Sekondari Mlali iliyoko wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma. Maoni: 0620 800 462.