Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb.) amepongeza Umoja wa Watangazaji Wakongwe wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ambayo kwa sasa inatambulika kama TBC kwa kuanzisha umoja huo ambao utapeleka salamu kuwa ni kazi ya kistaarabu na ni sekta muhimu.
Mhe. Nape ameyazungumza hayo leo jijini Dar es Salaaam wakati wa kikao chake na Wakongwe wa Tasnia ya Habari nchini waliowahi kutangaza RTD wakati na baada ya Uhuru ambao kwa sasa ni wastaafu na wanachama wa Umoja huo.
“Redio Tanzania Dar es Salaam ni tunu ya Afrika kwa sababu ni chombo kilichoshiriki harakati za kupigania Uhuru wa Bara la Afrika, kuna historia nyingi ambazo hazijatamkwa hivyo ni muhimu zikazungumzwa kwa kuwa wahusika bado mpo”, amesema Waziri Nnauye.
Ameongeza kuwa Serikali ipo tayari kuwashika mkono ili Umoja huo uweze kutekeleza maono yao ya kuanzisha redio na Chuo cha Utangazaji na kuna wadau wa Wizara hiyo ambao wanaweza kuvutiwa na wazo hilo pia na kuamua kufadhili.
Amesisitiza kuwa, zamani vyombo vya habari vilikuwa na vipindi vinavyojenga jamii lakini sasa vinaanza kupotea hivyo kuna umuhimu wa kushirikiana na wanatasnia hao katika kurithisha ujuzi ili kurudisha heshima ya tasnia na nchi kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Waziri Nape ameielekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuutambua Umoja huo kama wadau muhimu katika Sekta ya Habari na wawe wanapata mialiko katika shughuli mbalimbali za kisekta.
Aidha, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limetakiwa kuandaa vipindi na kufanya mahojiano na wakongwe hao wa RTD ili yale yote yaliyoleta heshima ya utangazaji katika nchi yetu yazungumzwe.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti Wakongwe hao wa RTD wamesema lengo la kuanzisha umoja huo wenye wanachama zaidi ya 200 ni kurejesha heshima ya Tasnia ya Habari nchini hasa katika utayarishaji wa vipindi, utafutaji wa vyanzo vya makala, uandishi wa skripti na matumizi ya Kiswahili fasaha katika utangazaji.
Sambamba na hilo wapo katika mchakato wa kuadhimisha miaka 73 ya utangazaji mwaka huu wa 2024 ili vijana waliopo kwenye tasnia ya Habari wajifunze na kujua historia ya utangazaji nchini.
Baadhi ya wanachama wa umoja huo ni pamoja na Rose Haji Mwalimu, Suleiman Kumchaya, Albert Msemembo, Angalieni Mpendu, Tido Mhando, Debora Mwenda, Eda Sanga, Godliver Rweyemamu, Judica Losai, Ally Said Tunku, na wengineo wengi.