Mratibu wa mradi wa HEET kitaifa Dkt. Kennedy Hosea akizungumza na Waratibu wa mradi wa HEET chuo kikuu Mzumbe
Mratibu wa eneo namba 4 la mradi wa HEET chuo kikuu Mzumbe Dkt.Albogast Musabila akieleza namna chuo kinavyoishirikisha kamati ya Ushauri wa kitasnia katika uandaaji wa mtaala mpya wa chuo kikuu Mzumbe
Naibu Mratibu wa mradi wa HEET chuo Kikuu Mzumbe Dkt.Hawa Tundui akizungumza katika kikao cha majadiliano natimu ya uratibu wa kitaifa ya mradi wa HEET
Dkt. Hosea akisistiza jambo kwa Naibu Mratibu wa mradi wa Chuo kikuu Mzumbe Dkt. Hawa Tundui
Timu ya uratibu wa mradi wa HEET kitaifa wakifuatilia michoro ya majengo ya chuo kikuu Mzumbe.
Waratibu wakifuatilia michoro ya majengo yanayotarajiwa kujengwa chuo kikuu Mzumbe Kampasi kuu Morogoro na Tanga kwa ufadhili wa mradi wa HEET
Picha ya pamoja ya Waratibu wa mradi wa HEET kitaifa wakiongozwa na Dkt. Kenedy Hosea (katikati) na timu ya chuo kikuu Mzumbe ikiongozwa na Dkt. Hawa Tundui
……………………
Mratibu wa kitaifa wa mradi wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi (HEET) unaoratibiwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ufadhili wa benki ya dunia Dkt. Kennedy Hosea amehimiza vyuo vikuu nchini vinavyonufaika na ufadhili wa mradi wa HEET kuzingatia uanzishwaji wa mitaala mipya ambayo itawapatia ujuzi unaoendana na soko la ajira la sasa na kuwawezesha wahitimu kujiajiri wao wenyewe.
Dkt. Hosea ameyasema hayo Machi 26 mkoani Morogoro alipokutana na kuzungumza na timu ya uratibu wa mradi wa HEET ya chuo kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro katika ziara yake aliyoambatana na Wataalamu wanaosimamia mradi huo kitaifa kwa lengo la kutoa usaidizi wa kitaalamu kwenye utekelezaji wa mradi kwa taasisi zinazonufaika na mradi huo
Ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kwa dhati kutatua changamoto ya ajira na kwamba kampasi zote mpya zinazoanzishwa nchini kupitia mradi wa HEET ni za kimkakati katika kukabiliana na changamoto hiyo na hivyo zina wajibu wa kuandaa mitaala tofauti na iliyopo sasa ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi utakaowawezesha kujiajiri na kuajiri wengine na kuleta mapinduzi ya kijamii na kiuchumi kwa taifa kupitia elimu watakayopata vyuoni
Dkt. Hosea amekipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa hatua kubwa iliyopiga kwenye utekelezaji wa mradi huo hususani kwenye eneo la ushirikishaji wa jamii na wadau katika hatua za awali za maandalizi ya ujenzi wa kampasi ya Tanga na uboreshaji na uanzishaji wa mitaala mipya zoezi ambalo bado linaendelea na kuwataka kuitumia zaidi kamati ya ushauri ya ajira na viwanda kwenye maandalizi ya mitaala
Kwa upande wake Naibu Mratibu wa mradi wa HEET wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Hawa Tundui amemshukuru Mratibu wa kitaifa na timu yake kwa kuweza kufika chuoni hapo na kujadiliana kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo na kuongeza kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kimepiga hatua kubwa kwani mtaala ulioandaliwa kwa ajili ya kampasi ya Tanga ni mpya kabisa wenye kozi zinazozingatia ujuzi na uwezo wa mhitimu kujiajiri na hivyo kuleta mapinduzi ya kiuchumi kama ilivyokusudiwa na mradi