Na. Abel Paul,Jeshi la Polisi-Moshi Kilimanjaro
Jeshi la Polisi Nchini limesema Machi 20, 2024 lilitoa taarifa kuhusiana na kifo cha Omary Saimon Msamo kilichotokea huko Wilayani Karatu Mkoa wa Arusha Machi 16, 2024.
Akitoa taarifa hiyo leo machi 26,2024 Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini Naibu Kamishna wa Polisi DCP David Misime amesema Jeshi hilo lilieleza mazingira ya tukio hilo ambapo amebainisha kuwa ilibidi kushirikisha wataalam mbalimbali wakiwepo wachunguzi wa matukio ya vifo.
DCP Misime aliendelea kueleza kuwa Timu ya uchunguzi wa tukio hilo ilipofanya uchunguzi wa tukio hilo ilibaini kuwa kifo chake hakikuwa cha kawaida bali ilikuwa ni Mauaji.
Aidha Msemaji wa Jeshi hilo alisema Baada ya kubaini hivyo Jeshi hilo lilianza uchunguzi wa mauaji hayo ambapo lilibaini waliohusika wa mauaji hayo.
Sambamba na hilo amebainisha kuwa uchunguzi umebaini kuwa malengo yalikuwa ni kumpora Omary Saimon Masamo chochote kile watakacho mkuta nacho.
Misime ameviambia vyombo vya habari kuwa Waliohusika na mauaji hayo tayari wamekamatwa na wamekutwa wakiwa na simu ya marehemu huku fedha walizompora kiasi cha Shilingi 200,000/= wakiwa tayari wameshagawana na kuzitumia.
Waliokamatwa ni Anthony Paskali ambaye anajulikana kwa jina maarufu Lulu na Emmanuel Godwin Jeseph anayejulikana kwa jina maarufu la Emma wote wakiwa ni wakazi wa Wilaya ya Karatu.
Taratibu zilizobaki za kiuchunguzi zinakamilishwa ili hatua nyingine za kisheria ziweze kufuata.
Pia DCP Misime amesema Jeshi la Polisi linaendelea kutoa tahadhari kwa baadhi ya watu kuacha kueneza taarifa za uwongo, chuki na uzushi dhidi ya mtu mwingine au taasisi kwa ajili ya malengo yao binafsi kwani kwakufanya hivyo watakuwa wanaukaribisha mkono wa sheria uweze kuwafikia na kuchukuliwa hatua.