Mratibu Mwandamizi wa Mradi, Kampuni ya SANLG World Investment Bw. Bahari Leo akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 25, 2024 Jijini Dar es Salaam.
Uongozi wa Kampuni ya SANLG World Investment wakiwa katika picha ya pamoja wakati wakizungumza na waandishi wa habari.
…………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Kampuni ya SANLG World Investment imejipanga kuwachukulia hatua kali za kisheria wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa ya Pikipiki kwa kutumia nembo ya SANLG, huku wakitoa wito kwa jamii kutoa taarifa endapo wataona mtu yoyote anauza au anatumia bidhaa feki ya Pikipiki ya SANLG.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 25, 2024 jijini Dar es Salaam, Mratibu Mwandamizi wa Mradi, Kampuni ya SANLG World Investment Bw. Bahari Leo, amesema kuwa wao ni wamiliki halali wa nembo ya biashara ya SANLG kwa kufata utaratibu zote ikiwemo kuisajili kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Bw. Leo amesema kuwa wataendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya kampuni yoyote ambayo itatumia vibaya nembo ya SANLG nchini Tanzania kutokana ni kinyume cha sheria.
“Tunatoa wito kwa watanzania kutoa taarifa endapo wataona pikipiki hizi, taarifa wanazotoa inapothibitishwa mauzo, jina la kampuni, namba ya mawasiliano, jina la mhusika na namba ya TIN, sisi tutatoa zawadi ya shilingi 200, 000” amesema.
Bw. Leo amesema kuwa uwepo wa pikipiki zenye nembo feki ya SANLG katika soko imesababisha kupungua kwa mauzo kwa kiasi kikubwa.
Mkurugenzi wa Route Marketing Bi. Anisa Nkulo amesisitiza umuhimu wa kutumia biadhaa halisi na kuepuka kutumia bidhaa feki kwani zinamadhara makubwa katika matumizi.
“Kuna bidhaa nyingi feki hasa bodaboda, zinatumika mikoani hasa vijijini kutokana na kukosa uwelewa wa kutambua bidhaa feki” amesema Bi. Nkulo
Bi. Nkulo amesema kuwa wakati mwengine chanzo cha ajali nchini imetokana na kutumia bidhaa ambayo ni feki, huku akitoa wito kwa watanzania kuacha kununua vitu vya bei ndogo bila kujilidhisha ubora wake ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.