Shirika lisilo la Kiserikali la Kilimanjaro Dialogue Institute (KDI) lenye makao yake jijini Dar es salaam linalofanya shughuli za kukuza na kudumisha amani na maridhiano, siku ya tarahe 24 Mwezi Machi lilifanya tukio maalum la kufuturisha waumini wa dini na madhebu tofauti ikiwa huu ni mwezi wa mfungo wa Kwaresma kwa waumini wa dini ya Kikristo na Ramadhani kwa waumini wa dini ya kiislamu. Shughuli hiyo, ambayo Mgeni wake rasmi alikuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Sheikh, Daktari Alhad Musa Salum, lenye kichwa cha habari “Karamu ya Amani: Iftar na Kwaresma” liliwaleta pamoja watu kutoka asili mbalimbali za kidini kushiriki chakula na kushiriki mazungumzo yenye malengo ya kuenzi amani tunayoifurahia watanzania.
Wakati wa chakula, wageni walikuwa na nafasi ya kushiriki katika mazungumzo ya kupitia miongozo na kushiriki katika tafakari juu ya umuhimu wa Ramadhani na Kwaresma katika imani zao. Tukio hilo lililenga kukuza uelewa, heshima, na mshikamano kati ya watu wa asili tofauti za kidini, likitilia mkazo umuhimu wa upendo na umoja katika jamii yenye watu wa imani tofauti. Akizungumza katika tukio hilo, mwenyekiti wa taasisi hiyo ndugu Ibrahim Yunus aligusia umuhimu wa kudumisha amani na aliwasisitizia Viongozi wa dini, wanahabari, wafanyabiashara, watafiti wa elimu, wanadiplomasia, viongozi wa tasnia za sanaa na michezo waliohudhuria hapo kushirikiana na serikali kudumisha amani ya taifa letu Tanzania.
“Tunafurahi kwa taasisi ya KDI kuandaa tukio hili lenye maana ambalo linaadhimisha utajiri wa mila zetu tofauti za kidini, na linaendana na dira ya upendo na maridhiano aliyotutengenezea rais wetu, mama yetu Mheshimiwa Dr. Samia Suluhu Hassan.” alisema Mwenyekiti wa JMAT Sheikh Alhad Musa Salum. Pia Mchungaji Christosiler Kalata ambaye ni mwenyekiti wa JMAT kwa mkoa wa Dar es Salaam alisema, “Kwa kukutana pamoja kwa chakula cha pamoja, tunatumai kuendeleza uelewa na thamani ya imani za kila mmoja, kukuza jamii yenye kujumuisha, yenye umoja, amani na maridhiano zaidi.”
Tukio hilo lilifanyika kwa msaada mkubwa wa taasisi isiyo ya kiserikali ya ISHIK na taasisi ya Umoja wa wafanyabiashara ya Tanzania Global Business Initiative.