Na Lilian Lundo – Maelezo
Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuliimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuwekeza zaidi ikiwemo kununua ndege ili kulifanya limudu kutoa huduma na kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi amesema hayo leo Machi 24, 2024, jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari pamoja na waandishi wa habari, kuhusu mafanikio ya miaka mitatu ya uongozi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Katika miaka mitatu, Serikali imenunua ndege tano zikiwemo tatu za masafa ya kati ambazo ni Airbus A220 mbili; Boeing 737 Max9; Boeing 767-300F ya mizigo na Dash 8 Q-400 na zote zinaendelea kutoa huduma,” amesema Bw. Matinyi.
Aidha, amesema kuwa ndege mbili zaidi, Boeing 737 Max9, ambayo iko katika hatua ya makabidhiano, na moja ya masafa marefu aina ya Boeing 787-8, ambayo ipo katika hatua ya uundwaji, tayari zimeshanunuliwa na zinatarajiwa kuwasili nchini mwezi Machi na Aprili mwaka huu.
Amesema kuwa, kwa kujumuisha na uwekezaji huu sasa ATCL ina jumla ya ndege za abiria 12 na moja ya mizigo zinazohuduma vituo 24 kutoka vituo 19 vya mwaka 2021 na inatarajiwa vitaongezeka.
Kwa ujumla wake, ATCL imeongeza abiria kutoka 537,155 mwaka 2021 hadi 1,070,734; tani za mizigo 1,290 mwaka 2021 hadi 3,561; na miruko 10,550 mwaka 2021 hadi 17,198 mwaka
2023.
Kwa upande wa ujenzi wa barabara, amesema kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu (2021-2024), Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imefanikiwa kukamilisha miradi 25 ya barabara yenye urefu wa kilometa 1,198.50.
Katika kipindi hicho, jumla ya barabara 57 zenye urefu wa kilometa 3,794.1, ziko hatua mbalimbali za utekelezaji.
Hali kadharika, miradi ya ujenzi wa madaraja makubwa nane imekamilika. Miradi mitano ya ujenzi wa madaraja inaendelea kutekelezwa na ipo katika hatua mbalimbali. Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa daraja la J. P. Magufuli (Kigongo – Busisi) mkoani Mwanza lenye urefu wa mita 3,200 kwenye ziwa Victoria likiunganisha mji wa Mwanza na mikoa ya Geita na Kagera.
“Serikali ya Awamu ya Sita imeongeza bajeti ya uboreshaji miundombinu chini ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na kufikia jumla ya shilingi trilioni 2.53 katika kipindi cha miaka mitatu. Fedha hizi zimewezesha ujenzi wa barabara za lami za kilomita 819.22, ambazo ni tofauti na barabara za lami zilizo chini ya TANROADS, na hivyo kuongeza mtandao wake kutoka kilomita 2,404.90 hadi 3,224.12,” amesema Bw. Matingi.
Kwa upande wa barabara za changarawe, jumla ya kilomita 11,924.36 zimejengwa na kuongeza mtandao wake kutoka kilomita 29,183.36 hadi 41,107.52. Pia, kumekuwa na ujenzi wa madaraja mengi nchini ikiwemo kutumia teknolojia ya mawe.