Madereva wanafunzi wa Magari ya mizigo, abiria na viongozi (VIP COURSE) wametakiwa kuzingatia na kufuata sheria, alama, ishara na michoro ya usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
Kauli hiyo imetolewa Machi 25, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Benjamin Kuzaga wakati akifingua mafunzo ya muda mfupi kwa madereva wa magari ya mizigo, abiria na viongozi katika Chuo cha udereva cha Agility Professional Driving School (APDS) cha Jijini Mbeya.
Aidha, Kamanda Kuzaga amewataka madereva wanafunzi kuheshimu watumiaji wengine wa barabara kwani nao wana haki ya kutumia barabara.
“Mbali ya vyombo vya moto kuna watumiaji wengine wa barabara, walemavu, watoto, wenye uoni hafifu na viziwi, hao nao wana haki ya kutumia barabara, waheshimuni kwa kuhakikisha mnafuata sheria, alama, ishara na michoro iliyopo barabarani ” alisema Kamanda Kuzaga.
Mkufunzi Mhandisi David Mtunguja kutoka chuo cha ufundi Arusha amesisitiza suala la umuhimu wa Dereva kulijua gari lake ili kuepuka ajali ambazo zaidi ya asilimia 70 zinasababishwa na uzembe wa madereva.
Aidha, Mkurugenzi wa Agility Professional Driving School Mhandisi Anthony Malamla ameomba Serikali kuongeza nguvu ya udhibiti wa vyuo vya udereva ambavyo havijakidhi vigezo wala kusajiliwa ili kuepuka utapeli na kuzalisha madereva wasio na weledi katika taaluma ya udereva.
Jumla ya madereva wanafunzi 16 wa magari ya mizigo, abiria na viongozi (VIP Course) kutoka mikoa ya Mbeya, Mwanza na Arusha wamefungulia rasmi mafunzo ya udereva ya muda mfupi katika chuo hicho kwa lengo la kuwajenga uwezo na weledi katika matumizi sahihi ya barabara.