Na Mwandishi Wetu, Morogoro
WADAU wa kilimo cha mazao ya viungo wameiomba serikali kutengeneza sera rafiki ya kukuza, kuzalisha na kusindika mazao hayo, ili yawe na soko zuri ndani na nje ya Tanzania.
Wadau walioshiriki walitoka katika Mamlaka ya Kuthibiti Mazao ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, halmashauri za wilaya, kampuni zinazosindika viungo na asasi za kiraia.
Mkutano huo uliazimia kwamba uwepo ubia wa kuwawezesha wadau katika sekta ya viungo kubadilishana maarifa, mbinu bora na uvumbuzi wa changamoto katika uzalishaji wa viungo, usindikaji na uuzaji.
Aidha, mkutano huo ulisisitiza kwamba ubia wa wadau uendeshwe kwa ufanisi na uwazi na kufikia lengo hilo mkutano zimetengenezwa adidu za rejea.
Mkutano umesisitiza muhimu wa Tanzania kuzalisha viungo vinavyohimili ushindani katika soko la ndani na la dunia.
Aidha mkutano umeazimia kwamba changamoto za uzalishaji, usindikaji, sera wezeshi, uhifadhi, upatikanaji wa taarifa za masoko ziainishwe.
Kadhalika mkutano umetaka kuanzishwa vikundi kazi au kamati za kushughulikkia maeneo maalumu kama vile uzalishaji, usindikaji, uuzaji na utetezi wa sera.
Mkutano uliazimia kwamba sekta binafsi inategemewa kuonesha ufanisi na uwazi katika kufanya biashara.
Wizara ya Kilimo imesisitiza umuhimu wa wadau kuunganisha nguvu kuimarisha uzalishaji wa mazao kulingana na mahitaji ya soko.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dk. Musa Ally Musa, alieleza kuwa mkoa huo una fursa za kuzalisha karafuu, mdalasini, iliki, na mchaimchai ambayo ni mazao yenye soko na bei nzuri.
Kwa upande wa karafuu, Dk Musa amesema kuwa mwaka 2023, mkoa umezalisha tani 2,000 za karafuu zenye thamani ya bilioni 36 katika Halmashauri ya Morogoro pekee.
“Hali ya hewa ni nzuri na ardhi ina rutuba jambo linaloibua fursa za kuzalisha mazao ya viungo kwa njia ya ufanisi na endelevu,” amesema
Naye Meneja wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Njanda ya Juu Kusani mwa Tanzania (SAGCOT) Kongani ya Kilombero, John Nakei amesema kutokana na ushirikiano na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro pamoja mwitikio wa wadau wa kilimo wamefanya mpango huo kufanikiwa.
“Tumejipanga vizuri kuhakikisha karafuu inazalishwa kwa wingi na ubora uleule ikiwemo kutoa mafunzo kwa wakulima na maofisa ugani,” amesema Nakei.