Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha ameishauri jamii kuhakikisha inadumisha utamaduni wa kuchangia damu kwakuwa ni jambo muhimu katika kuokoa afya za wahitaji.
Amezungumza hayo, mwishoni mwa wiki Kampasi kuu, Morogoro katika kilele cha siku ya Mzumbe na Kambi ya ujasiriamali iliyoambatana na upimaji Afya na uchangiaji damu katika zoezi lililoongozwa na Kituo cha afya Mzumbe kwa kushirikiana na Hospitali ya Jeshi Mzinga.
Profesa Mwegoha amesema kuchangia damu ni jambo la kheri na muhimu katika kuokoa afya na hivyo jamii inapaswa kushiriki ipasavyo katika shughuli zote za uchangiaji damu.
“Niwatie moyo wana mzumbe wenzangu na jamii tuchangie damu, ni jambo ni muhimu na la kheri katika kuokoa maisha” amesema.
Sambamba na hilo, kilele cha siku ya Mzumbe kiliambatana na mafunzo ya ukaguzi na fedha yaliyotolewa na kampuni ya Delloite inayojishughulisha na uhasibu, na ukaguzi kwa Wanafunzi wa fani ya uhasibu na fedha ili kuwajengea uwezo kwa kukutana na makundi yote na nyanja zote za kijamii hususani kutoa elimu ya kujiajiri, kuajiriwa, matumizi sahihi ya mitandao kwenye kujijengea uwezo,kupanua wigo wa kupata fursa na kukutana na mwanafunzi mmoja mmoja kwa mazungumzo ya kina.
Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali 2024 “Mzumbe Day and Entrepreneurship Camp” iliyofanyika Kampasi Kuu, Morogoro ilianza machi 20-22,2024 ikihusisha shughuli mbalimbali ikiwemo mbio, bonanza la michezo, kuwakutanisha wabunifu na wajasiriamali, sambamba na mawasilisho ya bunifu mbalimbali katika mabanda.