Tarehe 22 Machi 2024, Mhe. Phaustine Kasike, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Msumbiji alikutana na Gavana wa Jimbo la Zambezia, Mhe. Pio Augusto Matos kwenye Ofisi za Ubalozi zilizopo Jijini Maputo.
Wakati wa Mkutano huo, Viongozi hao wawili walizungumza masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Msumbiji.
Aidha, kupitia Mkutano huo, Mhe. Balozi Kasike alimueleza Mhe. Gavana Matos changamoto mbalimbali zinazowakabili Diaspora wa Tanzania waliopo Jimboni Zambezia na kumuomba asaidie katika kuzitafutia ufumbuzi.
Mhe. Gavana Matos alipokea ombi hilo na kumuahidi Mhe. Balozi Kasike kwamba Uongozi wa Jimbo lake utakutana na Watanzania hao hivi karibuni ili kujadiliana namna ya kumaliza changamoto zinazowakabili, lengo ikiwa ni kuimarisha uhusiano wa kihistoria na kidugu kati ya Tanzania na Msumbiji.
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania – Maputo
22 Machi, 2024