Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
SERIKALI Mkoa wa Singida imewataka watumishi wa umma na watu binafsi kutumia Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) katika kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwa unarahisisha utoaji na ufikishaji wa huduma kwa urahisi na kuondoa usumbufu wa kutumia gharama kufika katika ofisi za Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Singida,Godwin Gondwe, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alisema hayo jana wakati akifunga mafunzo kuhusu anwani za makazi kwa watumishi wa serikali,taasisi binafsi na viongozi wa dini yaliyofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.
Gondwe alisema suala la Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) linatakiwa kuchukuliwa kwa umuhimu wa kipekee sana kwani itafika wakati mtu anaweza kupata huduma serikalini au sehemu yeyote akiwa nyumbani kwake kwa kuingia kwenye mtandao wa NapA.
“Sisi kama viongozi wa serikali tunatakiwa kutoa huduma kwa wananchi kwa kutumia mfumo wa NaPA na mtakumbuka Rais Samia Suluhu Hassan amezengumzia sana kutatua kero na changamoto za wananchi na ametoa minara ili tuweze kuwahudumia wananchi kwa haraka kwani hivi sasa dunia inakwenda kwa kasi sana,” alisema Gondwe.
Alisema serikali imetengeneza mfumo wa NaPA ili kurahisisha huduma kwa wananchi hivyo unamhusu kila ambaye anafanya kazi serikali na asiye kwenye taasisi za serikali ambapo kwa watendaji wa kata mfumo huo utasaidia kupunguza siku za wananchi kupata huduma katika ofisi za kata.
Naye Mratibu Msaidizi w Anwani za Makazi Kitaifa kutoka Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Arnold Mkude,amesema katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kumeanzishwa utaratibu wa utoaji wa barua ya utambulisho lengo ikiwa ni kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidigitali.
Alisema hatua iliyofikiwa ya utoaji wa barua ya utambulisho ni kwamba majaribio yameanza kufanyika kuanzia mwezi Machi hadi Mei 2024 ambapo wadau katika suala hilo ni watendaji wa kata,mitaa,vijiji,watoa huduma na wananchi na lengo la majaribio hayo ni kubainisha mapungufu na changamoto ili kuboresha kabla ya kuanza matumizi nchi nzima.
Mkude alisema tangu operesheni Anwani za Makazi ianze zimeweza kukusanywa taarifa za Anwani za Makazi milioni 12. 8 na zimewekwa nguzo za majina ya barabara zaidi 222,000 na vibao vya namba za nyumba zaidi ya milioni 4.
Naye Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani ya Makazi kutoka Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Innocent Jacob, alisisitiza wananchi kuhakiki anwani zao na kutumia program tumizi ya umma (NaPA) kujua anwani zao kwani anwani za makazi ni fursa katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Mratibu wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani ya Makazi kutoka Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Jampyoni Mbugi amesema utumiaji wa mfumo huo utasaidia sana utoaji wa huduma na kuondoa matukio ya kiuhalifu kwa kuwa kila mtu atajulikana alipo.