ZAIDI ya vyanzo 20 vya maji vimehifadhiwa katika shamba la miti la Sao Hill lililopo wilaya ya Mufindi mkoani Iringa ambavyo vimekuwa vikihudumia miradi mikubwa na midogo ya wilaya na kitaifa.
Akizungumza wakati wa upandaji miti katika kata ya Bumilahinga kijiji cha Ulole,Mhifadhi mkuu wa Shamba la Miti Saohill PCO Tebby Yoram alisema kuwa uongozi wa shamba la miti Sao Hill wamekuwa mstari wa mbele kuhifadhi vyanzo vya maji kwa manufaa ya taifa.
PCO Yoram aliwaomba wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji kwa manufaa ya vizazi vya sasa na baadaye kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Lakini pia PCO Yoram alisema kuwa katika kuadhimisha siku ya upandaji miti shamba la miti Sao Hill walipanda zaidi ya miti 2000 rafiki na maji katika kata ya Bumilahinga kwa kuzunguka vyanzo vyote vya maji.
Kwa upande wake Mgeni rasmi katika zoezi la upandaji miti,Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Dkt. Linda Salekwa alisema kuwa misitu ni sehemu kubwa ya maisha ya wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwa imekuwa ikichangia kwa asilimia kubwa uchumi wa Mufindi.
Salekwa aliwataka wananchi wa Wilaya ya Mufindi kuhakikisha wanaitunza miche iliyopandwa na inayoendelea kupandwa kwenye vyanzo vya maji ili kuvilinda vyanzo hivyo kwa ajili ya vizazi vya sasa na baadaye.
Alisema kuwa wananchi wa wilaya ya Mufindi wanatakiwa kuendelea kupanda miti ya aina zote ili kulinda haki ya hewa nzuri iliyopo katika wilaya hiyo.
“Kwa namna ya pekee niwapongeze TFS kupitia Shamba La Miti Saohill wamekuwa wakifanya kazi kubwa sana ya kupanda miti na kutunza misitu lakini pia wameendelea kuwa mstari wa mbele kutuhamasisha kupanda miti ya kutosha katika maeneo yetu”