Baadhi ya wanafunzi wa shule ya sekondari Ruvuma Lutheran iliyopo wilaya ya Songea mkoani Ruvuma,wakiwa na miche ya miti kabla ya kuanza kwa zoezi la kupanda miti katika shule hiyo chini ya ufadhili wa shirika la kimataifa la Uhifadhi mazingira(WWF-Tanzania) na wakala wa misitu ncihini TFS Wilaya ya Songea.
………
Na Mwandishi maalum, Songea
SHIRIKA la Kimataifa la Uhifadhi Mazingira(WWF-Tanzania)kupitia mradi wa Uhifadhi mazingira(Faith Based Restoration Project) kwa kushirikiana na viongozi wa Dini wa mikoa ya Kusini,limepandamiti miti zaidi 300 katika shule ya sekondari Ruvuma Lutheran wilaya Songea mkoani Ruvuma.
Afisa program wa misitu kutoka WWF James Wumbura alisema,hatua hiyo ni kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita ya kuhifadhi mazingira na kurudisha uoto wa asili ulioharibiwa kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo kilimo na ufugaji.
Alisema,zoezi la kupanda miti limetanguliwa na mafunzo ya siku mbili ya kuwajengewa uelewa viongozi wa dini kuhusu wajibu wa taasisi za dini na umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa kutumia mwongozo wa vitabu vitakatifu yaani Biblia na Quran.
Alisema,mpango wa upandaji miti ni endelevu na litafanyika katika mikoa mingine ya Lindi na Mtwara ambapo takribani ekta 400 zitapandwa miti aina mbalimbali kupitia taasisi za dini katika mikoa ya kusini,ili kuokoa ekta zaidi ya milioni 5.2 za miti ifikapo mwaka 2030.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania mkoa wa Ruvuma Fulko Hyera alisema,viongozi wa dini katika mkoa wa Ruvuma wameanza kutafsiri vitabu vya Quran na Biblia inayozungumzia suala la uhifadhi wa mazingira ili kuleta uhalisia wa maeneo yaliyoathiriwa kutokana na mahitaji ya watu.
Alisema,hapo mwanzo Dunia ilikuwa mahali pazuri pa kuishi kwa kuwa na miti mingi mizuri,mito na ndege ambavyo ni rafiki mkubwa wa mazingira,lakini kwa sasa imeharibiwa na siyo rafiki tena.
Alisema,mpango wa kupanda miti ni unakusudia kuikumbusha na kuifundisha jamii na kutoa ujuzi kwa kizazi cha sasa kuhusu umuhimu wa kupanda miti katika maeneo yao ili kunusuru mazingira yetu kugeuka jangwa.
Alisema,kupitia viongozi wa dini watahakikisha wanarudisha uoto wa asili kwa kupanda miti,kuhifadhi mazingira na kulinda vyanzo vya maji ili dunia irudi kuwa mahali pazuri na sehemu salama kwa ajili ya kuishi Binadamu na viumbe wengine.
Alisema,kupitia elimu waliyopata viongozi wana jukumu kubwa la kuelimisha waumini na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanakwenda kuotesha miti na kila mmoja anashiriki katika utunzaji wa mazingira katika eneo lake.
Naye mwakilishi wa Bakwata kutoka mkoa wa Lindi Shekhe Said Salum alisema,mafunzo waliyopata ni kama ukumbusho tu kwani walishaagizwa kupitia vitabu vitakatifu kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira katika maeneo yao.
Alisema,uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji ni vitu ambavyo kwa kiasi kikubwa vimesababishwa na binadamu kutokana na harakati zao za maisha,kwa hiyo wana wajibu mkubwa kuhakikisha wanarudisha uoto wa asili kama walivyoagizwa na Mwenyezi Mungu kupitia kitabu cha Quran.
Askofu wa kanisa la KKKT Doyasisi ya Ruvuma Amon Mwenda,ameipongeza WWF kwa kutoa mafunzo kwa viongozi wa dini kwani yatasaidia kuikumbusha jamii umuhimu wa kutunza na kuhifadhi mazingira.
“Faida za kuhifadhi mazingira ni nyingi sana kwetu sisi binadamu ikiwemo kubakisha uoto wa asili,kupungua kwa magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa hewa safi na kuongeza uzalishaji wa chakula katika nchi yetu”alisema Askofu Mwenda.
Mwanafunzi wa shule ya sekondari Ruvuma Lutheran Agnes Msigala,ameishukuru WWF kwenda kupanda miti katika shule yao kwani miti iliypandwa itawawezesha kuwa na mazingira mazuri, kupata hewa safi na kuitumia miti hiyo kujifunza kwa vitendo katika masomo yao.