Na Sophia Kingimali.
Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila amepokea msaada wa taulo za kike na za watoto zenye thamani ya milioni 30 kwaajili ya kusaidia watoto na wazazi katika hospitali ya taifa Muhimbili huku akitaka wadau kuendelea kusaidi na katika hospitali nyingine kwani mahitaji bado ni mengi.
Akizungumza kwenye hafla ya kupokea msaada huo kutoka kwa kampuni ya Dowei Care leo Machi 22,2024 katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es salaam amesema msaada huo umekuja muda muafaka kwani kitengo hiko kina mahitaji mengi.
Amesema serikali inatambua juhudi zinazofanywa na sekta binafsi katika kuwahudumia wananchi hivyo ameimba kampuni hiyo kuangalia na namna nyingine ya kuweza kusaidia miundombinu katika hospital na vifaa tiba.
“Tunaomba kama kampuni kuangalia namna ya kuweza kusaidia na miundombinu ikiwemo vifaa tiba kama vya upasuaji kwani kwa kufanya hivyo kutaisaidia kuipunguzia gharama serikali kununua vifaa tiba lakini na hili la kugawa hizi taulo liendelee na kwa hospital nyingine”,Amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi mtendaji wa Hospital ya Muhimbili Profesa Mohamed Janabi ameishukuru kampuni ya Dowei huku akitoa rai kwa kampuni na taasisi nyingine kujitokeza kusaidia juhudi za serikali katika sekta afya hasa watoto,mama wajawazito na wazee.
Sambamba na hayo Profesa Janabi ameimba serikali kuangalia uwezekano wa kitengo cha watoto katika hospitali hiyo kiweze kujitegemea na kuwa hospitali kamili kwani kimekidhi haja ya kuwa hospitali kamili.
“Tunamshukuru sana Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa na uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya amewekeza pesa nyingi ambazo zimeleta matokeo chanya kwa mustakabari wa afya za watanzania”,Amesema Prof.Janabi.
Naye,Mkurugenzi mtendaji wa Dowei Care Victor Zhang amesema wao wameamua kurejesha shukrani kwa wateja kwa kuwekeza kwenye kusaidia umma hivyo wamejipanga kushirikiana na serikali kuhakikisha wanawafikia wanachi wengi.